Polisi wamsaka aliyesambaza video kumdhalilisha waziri

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 12:16 PM Apr 27 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP)   Pius Lutumo.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Pius Lutumo.

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamsaka mtu aliyerekodi video iliyokuwa ikimwonyesha Waziri na Mbunge Mstaafu wa Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa, akidhalilishwa kwa maneno, vitisho, dharau na kutishiwa kufungwa pingu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP)   Pius Lutumo, alisema jana katika taarifa yake kwamba mtu huyo anayetuhumiwa kusambaza video hiyo ikimwonyesha Dk. Kawambwa na mwenzake Cathbert Enock kwenye mitandao ya kijamii, ajisalimishe katika kituo cha polisi Bagamoyo.

Katika taarifa hiyo aliyoitoa  kwa waandishi wa habari mjini hapa, alisema tukio hilo lilitokea Aprili 24, mwaka huu,  majira ya saa 8:00 mchana  katika kijiji cha Kitopeni wilayani Bagamoyo.

SACP Lutumo alisema mtuhumiwa huyo alisambaza video hiyo iliyokuwa na maneno ya kumdhalilisha Dk. Kawambwa kwamba: “Shukuru Kawambwa Waziri wa Miundombinu enzi hizo, sasa dalali wa viwanja Bagamoyo na mhalifu wa kawaida'.

Alisema katika tukio hilo, Diwani Mstaafu  wa Kiromo, wilayani Bagamoyo, Hassan Usinga, na askari mgambo, Abdallah Mgeni, waliwashambulia Dk. Kawambwa na wenzake kwa maneno huku wakilazimisha wafungwe pingu.

Chanzo cha tukio hilo kinaelezwa kuwa ni magari ya mchanga ya mtuhumiwa kuharibu barabara na mashamba ya watu yakipita katika eneo hilo hali iliyosababisha wananchi kufunga barabara kwa magogo kuzuia uharibifu kuendelea.

Kamanda Lutumo alisema watuhumiwa hao wawili, Usinga na Mgeni, walikamatwa na polisi na baadae kuachiwa kwa dhamana kwa mujibu wa sheria na  watafikishwa mahakamani uchunguzi ukikamilika kuhusiana na tukio hilo.

Mbali ya tukio hilo kuelezea kutokea Aprili 24, mapema Aprili 25, video ya tukio hilo ilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikimwonyesha mtuhumiwa akimtolea maneno makali na ya dharau Dk. Kawambwa.