Wazazi wanaoozesha wanafunzi wabanwa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 11:58 AM May 09 2024
Wazazi wanaoozesha wanafunzi kukiona cha moto.
Picha: Maktaba
Wazazi wanaoozesha wanafunzi kukiona cha moto.

KAMATI ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Kata ya Mwamala mjini hapa imedhibiti utoroshwaji wanafunzi wasichana na kuozwa kinyume cha sheria, imeelezwa.

Hayo yameelezwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata hiyo, Sophia Philbert wakati akizungumza na Nipashe kuhusiana na hali ya ukatili katika kata yake kufuatia utekelezaji wa Mradi wa Wanajamii na Vyombo vya Habari katika kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ufadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT).

Sophia, amesema wamekuwa wakipata taarifa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutoka kwa walimu wakuu wao kuwa hawajulikani walipo hasa wasichana.

Amesema wakuu wao hao, wamekuwa wakifuatulia wanabaini wameozeshwa na wazazi wao kwa kulipwa mahari ya ng’ombe.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Suzana Kayange, amesema wameingia makubaliano ya pamoja ya kukagua umri wa kila anayeolewa kwenye cheti cha kuzaliwa na kadi ya kliniki ili kukabiliana na ndoa na mimba za utotoni ambazo kwa kiwango kikubwa zinakatisha ndoto za wanafunzi kupata elimu.

Amesema kabla ya kuweka utaratibu huo, wasichana wenye umri chini ya miaka 18 walikuwa wakiolewa bila kufuata taratibu  kimya kimya baina ya wazazi kwa wazazi baada ya kulipana mahari.

Amesema baada ya utaratibu huo kuanza, hakuna tena ndoa za utotoni na wanafunzi wasichana wanaendelea na masomo.

Mmoja wa wajumbe wa MTAKUWWA, Ramadhani Mahona, amesema ili wawafike wananchi wengi na kuwaelimisha wanatakiwa kuwezeshwa usafiri wa baiskeli na vocha kwa ajili ya mawasiliano ili kupeana taarifa.

Amesema kama mpango wa serikali na mashirika ni kutokomeza ukatili, waangalie namna ya kuziwezesha kamati za MTAKUWWA za kata kufanikisha malengo yao.