Kauli za upotoshaji za Tundu Lissu hazivumiliki

By Christina Haule , Nipashe
Published at 12:53 PM May 09 2024
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu.
Picha: Maktaba
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani Morogoro, kimekitaka chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kuacha tabia ya upotoshaji kwa wananchi na ubakaji wa taarifa na michakato ya mafanikio ya nchi inayofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Katibu wa Siasa, Uenezi na mafunzo CCM mkoani hapa Zangina Shanang anasema kauli za upotoshaji zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu wakati wa mkutano wa hadhara mwezi Aprili mwaka huu hazivumiliki.

Zangina amesema agenda ya uwepo wa Serikali ya tatu ya Tanganyika kuwa ni TAMISEMI sio hoja ya msingi sababu haipo na TAMISEMI ni Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa ambayo ipo ndani ya Serikali Tanzania.

Ameitaka CHADEMA kutolazimisha agenda ya serikali tatu ionekane ni hitajio la wananchi wakati ni mpango wa CHADEMA wa kuongeza utitiri wa madaraka kwa kutaka kujiimarisha kisisasa na kisha kuuvunja Muungano kwa kuwa wamejaa roho ya ubaguzi kwa Zanzibar.

Amesema watanzania wanapaswa kutambua kuwa mpango wa Serikali ya Tanganyika uliibuka kwenye katiba ya Tume ya Jaji Warioba kwa kuwa UKAWA waliubaka mchakato wa tume hiyo na kuiaminisha kuwa ilikuwa inakusanya maoni ya wananchi lakini kiuhalisia CHADEMA ilipita kila mkoa kupandikiza watu ili waingize misimamo yao.

Hivyo amewataka CHADEMA kuacha kulazimisha kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika itakayoongeza mzigo wa kodi kwa watanzania sababu Serikali mbili zinatosha ambapo alisema kama wanataka Serikali tatu waanze na kubadilisha kwenye salamu yao kwa kuonesha vidole vitatu badala ya viwili na sio kuwarubuni wananchi.

“kiukweli kama CHADEMA hawauoni wema wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan basi wana matatizo ya ufahamu maana wameshasahau ugumu wa kisiasa walioupitia miaka mitatu iliyopita, na sasa mama anastahili kupewa maua yake ya pongezi kuu “ amesema Zangina.