Ummy: Tunaimarisha huduma NCD's hadi ngazi ya zahanati

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:15 PM Apr 26 2024
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

TANZANIA imeweka wazi mipango ya nchi katika kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD's), kushirikiana na wadau, kuongeza wigo wa kutambua, kuyatibu na kutoa elimu dhidi ya magonjwa hayo hadi ngazi ya zahanati.

Imesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo kwenye orodha ya nchi barani Afrika zinazoendelea, zenye takwimu kubwa ya wanaougua NCD's, huku serikali ikibeba mzigo wa matibabu hayo kama vile figo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliyasema hayo jIjini Dar es Salaam, akifungua kongamano la kimataifa barani Afrika dhidi ya NCDs ‘PEN Plus’, lililokutanisha washiriki 300 kuazimia mbinu kukabili, kisukari aina ya kwanza, selimundu na magonjwa ya moyo kwa watoto 

Alisema kwamba nchini NCD's, huchangia takribani asilimia 70 ya magonjwa mengine kama vile figo na moyo, akisema asilimia tisa ya Watanzania wanaugua kisukari huku asilimia 15 wanaugua presha.

“Lengo la dunia ni kufikia angalau theluthi moja kupunguza NCDs, asilimia 77 ya NCD's ipo katika nchi za uchumi kati na mdogo. Zipo hatua tunachukua kama nchi kwa kuhimiza ufanyaji mazoezi, kutoa elimu kubadili mtindo wa maisha, kufanya vipimo.

“Vilevile kama nchi tunahimiza utolewaji wa chanjo ya HPV (chanjo la saratani ya mlango wa kizazi), kwa watoto wenye umri kuanzia miaka tisa hadi 14, ili kuwakinga na ugonjwa huu ambao inaathiri sana,” alisema Ummy.

Alisema serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za afya nchini, ili kutoa matibabu sahihi kwa wakati, alionya matumizi ya vilevi kama pombe, akisema huongeza kasi ya NCD's.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini, Dk. Charles Sagoe-Moses, alisema NCD's, husababisha mamilioni ya vifo kwa mwaka, ambavyo vingeweza kuepuka, kutokana huduma duni kukabili magonjwa hayo.

“Takribani vifo 100,000 husababishwa na sababu nne; kisukari aina ya kwanza, selimundu, magonjwa ya mfumo wa hewa na moyo kwa watoto. Katika nchi nyingi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, huduma za matibabu kwa NCD's hupatikana tu kwenye hospitali za rufani.

“Waru wengi na familia zao wanakumbana na gharama kubwa za matibabu haya au zile za usafiri kwenda na kurudi, kuoata huduma na kusababisha ulemavu ama vifo,” alisema Dk. Charles.

Alisema kwenye nchi hizo watoto wakigundulika kuwa na kisukari aina ya kwanza, uwezekano kwa kuishi ni kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja, ikilinganishwa na nchi zilizoendelea ambao uwezekano ni hadi umri wa kati.

“Kila siku watoto wa Kifarika 1000 wenye selimundu huzaliwa. Bila ya kuwa na hydroxyurea (moja ya tiba), ambayo ni tiba iliyodumu kwa takribani muongo mmoja, nusu ya watoto hawa watafariki kutokana na ugonjwa huu kabla ya kufikishwa miaka mitano.

“Asilimia 20 ya wenye umri wa miaka tisa kwenye nchi za uchumi chini ambaye pengine angepona kwa magonjwa ya mfumo wa hewa, atafariki akiwa na miaka sita,” alieleza Dk. Charles.

Mwenyekiti wa Mtandao wa NCDI Poverty, Dk. Gene Bukhman, alisema mradi wa PEN unatekelezwa kwenye nchi 76 duniani, ikiwamo kutoka barabani Afrika, kujikita katika Katia kukabiliana na NCD's.