Wanafunzi msingi, sekondari watoroshwa kwenda kuchunga

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 03:05 PM Apr 29 2024
Wanafunzi watoroshwa kwenda kuchunga.
PICHA: MAKTABA
Wanafunzi watoroshwa kwenda kuchunga.

WAZAZI na walezi wenye wanafunzi wanaosoma shule za msingi na sekondari Kata ya Mwamala Halmashauri ya Shinyanga, wanadaiwa kuwatorosha watoto wao wa kiume na kuwasafirisha katika mikoa ya Rukwa na Tabora kufanya kazi za kuchunga mifugo.

Pia, baadhi yao wamekuwa wakiwashawishi wanafunzi wa kike kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho hasa ya darasa la saba ili wafeli na kubaki nyumbani na kusaidia shughuli za kilimo, wengine kuozeshwa.

Hayo yameelezwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igegu, Leme Solo, wakati akizungumza na Nipashe.

Pamoja na mambo mengine Leme ameeleza namna wanavyoshirikiana na wazazi katika kukabiliana na tatizo la utoro kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanamaliza masomo yao salama na kutimiza ndoto zao.

Amesema wanafuzi wa kiume wanaongoza kwa kuacha masomo kulinganisha na wanafunzi wa kike na wanapofuatilia wanakuta wazazi wao wamewatorosha na kuwapeleka katika mikoa ya Rukwa na Tabora kufanya kazi ya kuchunga mifugo.

 Amesema, wanafunzi wa kike wao wamekuwa wakirubuniwa kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho ili wasifaulu na kuendelea na masomo yao na wengi wanakubali na kuandika majibu ambayo siyo sahihi na matusi.

 Amesema kwa wanafunzi wanaofaulu wazazi wanagoma kuwapeleka sekondari kwa kigezo hawana uwezo wa kuwasomesha.

“Wanafunzi wanaofanya haya na kutoroshwa ni wale wanaotoka katika mazingira magumu na wengi unapowafuatilia unakuta wanalelewa na mzazi mmoja au ndugu zao, hivyo anakosa mtu wa kumsukuma kuendelea na masomo,” amesema.

Mwalimu wa malezi katika Shule ya Sekondari ya Kaselya, Theodora Mdagachule amesema kuna wazazi wamekuwa wakitumia mifano ya waliohitimu elimu za vyuo vikuu wakisema wako mitaani kwa kukosa ajira.

 Amesema kwa ukubwa wa tatizo hilo wameanzisha klabu za wanafunzi shuleni ambapo wanawakutanisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kujadili mambo mbalimbali yanayowakabili ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa elimu.

 Amesema wengi wao wameelimika na wamekuwa wakiwafikishia malalamiko kutoka kwa wazazi wao hasa wanapolazimishwa kuolewa, kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwamala, Suzana Kayange amesema amekuwa akishirikiana na Kamati ya Mtakuwwa, watendaji wa vijiji na wenyeviti wa serikali za vijiji kuwaelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu.