Wanafunzi wahofiwa kufa basi kutumbukia korongoni

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:03 AM Apr 13 2024
Baadhi ya wananchi wakiangali mabaki ya gari yenye namba za usajili T 496 EFK aina ya Toyota Hiace la shule ya msingi Ghati Memorial ya jijini Arusha, wakati likitolewa kwenye Mto Mbasi, Mtaa wa Engosingiu, Kata ya Sinoni jana,baada ya kuzama katika mto.

WANAFUNZI saba hawajulikani waliko mpaka sasa, huku mmoja kati yao ameopoliwa akiwa tayari amepoteza maisha, baada ya basi dogo la wanafunzi la Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya ‘Ghati Memorial ya jijini Arusha, kuzama kwenye korongo lenye maji mengi yanayotokana na mafuriko ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha.

Basi hilo aina ya Toyota Hiace, lilizama jana, majira ya saa 12 asubuhi katika korongo lililoko eneo la Engosheratoni, kata ya Sononi baada ya kuvutwa na maji hayo yaliyokuwa yamevuka kimo cha daraja.

 Jana, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa, alithibitisha kuwa basi hilo lilikuwa na watu 13, kati yao 11 wakiwa wanafunzi wa shule hiyo.

 “Hali si shwari kama mlivyosikia na kama ulivyojionea. Gari la Ghati Memorial School limetumbukia kwenye mto (korongo). Ilikuwa ni majira ya saa 12:00 asubuhi.

 “Mnafahamu kabisa kwamba mvua zilikuwa ni nyingi sana kuanzia usiku mpaka alfajiri mvua zilikuwa zinanyesha. Lakini wakati dereva anapita watu walimuambia kwamba haya maji huwezi kukatiza.

 “Dereva aliendelea kukaidi akalazimisha, baada ya kulazimisha alivyoingiza gari tu likavutwa likaingia mtoni. Gari lilikuwa na jumla ya watu 13, wanafunzi walikuwa 11, dereva mmoja na matroni mmoja ambaye ni mwalimu. Waliookolewa jumla yao ni watano, wanafunzi wakiwa watatu, dereva mmoja mwalimu mmoja,” alisema.

 Kwa mujibu wa Mtahengerwa, hadi jana mchana, waokoaji walikuwa wameuopoa majini mwili wa mwanafunzi mmoja ambaye kwa bahati mbaya walikuta amepoteza maisha.

 Kuhusu  uokoaji, Mkuu huyo wa Wilaya alisema: “Kwa hiyo kazi inayofanyika sasa hivi ni kuendelea kuhamasisha wananchi kuambaambaa na huu mto ili tuweze kujua wenzetu saba ambao hatuwaoni wako wapi. Kwa wale ambao hatujawapata wako wapi, tuendelee kuwa wavumilivu.”

 Mbunge wa Arusha (CCM), Mrisho Gambo, akizungumzia tukio hilo, alisema changamoto ya eneo hilo ni ya muda mrefu na wanaostahili kutupiwa lawama kutokana na ajali hiyo ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaozuia kujengwa kwa daraja eneo la Sinoni ilipotokea ajali.

 “Changamoto iliyokuwepo wenzetu wa TANESCO wamekuwa wanakataa daraja lisijengwe.  Hata ukienda kule kwenye kata ya Lemara pia tumepata mpaka fedha za kujenga daraja lakini TANESCO wanakataa. Cha kushangaza hata kama daraja hakuna wananchi wanapita, magari yanapita.

 “Sasa tumepata madhara makubwa kama haya, ni vizuri wenzetu waone watoto saba hawaonekani, mmoja ameokolewa amekufa na wengine wamekuwa majeruhi.

 “Hatuwezi kuzuia kitu kwa sababu tu ya sababu zao, wakati maisha ya watu yanapotea. Kwa hiyo mimi ombi langu kwa serikali, kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambao wanashughulika na maafa nchini.

 “Tuhakikishe kwamba wenzetu wa TANESCO wanatumia busara na hekima ili watoe fursa kwa wenzetu wa TARURA (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) wajenge daraja hapa na tuokoe maisha ya watoto wetu; maana hili jambo ni jambo kubwa, ni jambo gumu na ni masikitiko makubwa sana katika Jiji letu, lakini lakini pia katika Jimbo letu la Arusha,” alisema. 

 Gambo alisema kimsingi, wakiwa wawakilishi wa wananchi walishajenga hoja tayari, na hata ukienda kwenye Kata ya Lemara, ambayo inaunganisha na Kata ya Sinoni, kuna daraja moja linaitwa daraja la Nakiete.

 “Tuliongea na watu wa TARURA makao makuu, wakatuma timu kutoka mpaka ngazi ya taifa wakaja wakadizaini daraja (wakasanifu), bajeti ikatengwa lakini TANESCO wakaja baada ya kuona kuna bajeti ya serikali, wakaweka bango la kuzuia kivuko kisijengwe.

 “Kivuko ambacho kinatumika na wananchi kuna wafanyakazi wengi wanafanya kazi kule Sun Flug na maeneo mengine wanatumia hiyo njia kupita lakini leo TANESCO wanazuia,” alisema. 

 Hapa kwenyewe (Sinoni) tunajenga hoja kila siku. Wenyeviti wa serikali za mitaa wamejenga hoja, diwani wa kata hii amejenga hoja na wananchi imekuwa ni kilio chao cha siku nyingi lakini watu wa TANESCO wamekuwa ni kikwazo,” aliongeza. 

 Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Fedrick Kikukwa, alisema wanaiomba serikali kuwasaidia kujenga daraja katika barabara hiyo ya Sinoni/Lemara na si kivuko kwa sababu maafa yanayojitokeza yatakuwa makubwa zaidi.