Mambo muhimu katika kuanzisha biashara

By Magabilo Masambu , Nipashe
Published at 11:33 AM May 05 2024
Mambo muhimu katika kuanzisha biashara.
PICHA: MAKTABA
Mambo muhimu katika kuanzisha biashara.

LEO katika safu yetu, tuzungumze kuhusu biashara kidogo. Hii ni kwa sababu biashara ni Maisha. Kwa maana nyingine, maisha hayajakamilika bila kuuza na kununua. Lakini zaidi, wataalamu wa fedha wanasema kama huuzi chochote basi katika hatua za kuelekea kwenye mafanikio, utakuwa unazisikia tu kwa majirani.

Kwanza, tutakubaliana kwamba biashara yoyote huwa inaanza na wazo, lakini wazo bora lazima liwe limekusudia kutatua changamoto za jamii. Mfano, umepata wazo la kuuza maji, maana yake unatakiwa kujua kama hilo ni tatizo katika eneo hilo.

Kwa hiyo jambo la kwanza kabisa, unapotaka kuanzisha biashara, unatakiwa kufanya utafiti au uchunguzi mdogo kuhusiana na wazo lako la biashara. Utafiti huo utakuwa juu ya kutaka kufahamu changamoto kubwa waliyo nayo wananchi wa eneo hilo.

Biashara yoyote ambayo haitatui changamoto ya wakazi husika hata kama ungeifanya kwa miaka 100, hakuna siku utafanikiwa. Hii ni kwa sababu kama jambo uliloanzisha si hitaji la watu, maana yake hutapata wateja wa kununua bidhaa zako. Badala  yake watafuata bidhaa ambazo ni hitaji lao. 

Utafiti utakuwezesha kufahamu wateja wako watakuwa kina nani. Usianzishe biashara kwa kutegemea yeyote atakayepita atanunua, ndiyo yeyote atakayepita anaweza kununua lakini wale wateja wako uliowakusudia waendelee kuwepo.

Jambo la pili, epuka sana kuanzisha biashara inayofanywa na wengi katika eneo hilo. Unaweza kuwa unaishi mahali fulani, jirani yako anauza vitumbua na wewe ni mmoja wa wateja wake. Lakini kila siku unaona wateja ni wengi sana, wazo linalokuja kichwani mwako ni kwamba na mimi nikianzisha hapa, nitawapata kama yeye. Kitakachotokea kama utaanzisha maana yake mtagawana wateja. Kama alikuwa anapata Sh. 10,000 kwa siku, mtagawana na mwisho wa siku wote mtashindwa kuendelea na biashara.

Jambo la tatu, usianzishe biashara ambayo hujawahi kuifanya kwa pesa za mkopo. Siku hizi umekuja mtindo wa vikoba, kupeana pesa kila baada ya muda fulani au unaamua kwenda benki kukopa fedha kwaajili ya biashara ambayo ni ngeni kwako, hakika utajuta hapo baadaye usifanye hivyo.

Anza na mtaji mdogo ulio nao. Kwanza, utaanza kujifunza namna unavyopata faida hata kama ni kidogo lakini ukiweza kutunza hiyo faida ndogo na ukaweza kuikuza, basi katika biashara kubwa pia utafanya hivyo. Unapoanzisha biashara usiyo na uzoefu nayo, wakati huku kwenye kikundi au benki wanasubiri marejesho, kuna hatari ya kushindwa biashara hiyo na kuna wakati unaweza kugombana na wateja, ukidhani tatizo ni wao. Hatukatai kukopa ni jambo jema, lakini kopa wakati biashara tayari unaifahamu unajua faida yaze na wateja wako.

Jambo la nne, utamaduni na hali ya eneo. Bidhaa utakazouza lazima uzingatie utamaduni na hali ya eneo husika. Usifunguwe biashara tu kwa sababu unataka kuonekana kwamba na wewe ni mchakalikaji na kwamba wenzako wakienda kazini na wewe unakwenda kwenye biashara, unaona aibu kubaki nyumbani bora ukae kwenye duka hata kama hakuna wateja.

Huwezi kufanya biashara ya nguruwe maeneo ambayo yametawaliwa na jamii ya Waislam au ukafanya biashara ya kanzu maeneo ambayo yametawaliwa zaidi na Wakristo au unafanya biashara za makoti ya baridi Dar es Salaam.

Jambo la tano ni kuhusu uhakika wa bidhaa zenyewe. Kwanza, uhakika katika ubora, pili uhakika wa namna rahisi ya kuzipata kwa mwendelezo. Kwenye ubora wa bidhaa utakufanya uwe na wateja wa kudumu, wakishakuwa ni wa kudumu, maana yake hizo bidhaa zinatakiwa pia ziwe zinapatikana wakati wote. Hakuna jambo baya kwa mteja kumwambia bidhaa zimeisha njoo siku fulani ujuwe huyo ushamkosa.

Jambo la sita, kabla ya kuanzisha biashara uwe na uhakika wa lugha utakayokuwa unaitumia kwa wateja wako, bila kujali kwamba ni wachache au watakuwa wengi kiasi gani. Watanzania wengi tulivyo, huwa biashara ikiwa mpya na tupo katika harakati za kutafuta wateja huwa tuna tumia lugha nzuri sana, lakini tukishaona wateja wamezidi tunaanza lugha za dharau.

Mwisho kwa leo, ni juu ya matumizi ya fedha za biashara. Biashara nyingi zina faida kidogo, hivyo zinahitaji nidhamu ya hali ya juu, juu ya matumizi ya fedha. Ukiwa unafanya biashara huwezi kujua kwamba utafilisika ni mpaka utakapofirisika, kwasabahu mtaji na faida inatabia ya kujichanganya pamoja. Huwa si rahisi kujua matumizi unayofanya tayari unatumia mtaji ni mpaka uishiwe. 

0689157789

[email protected]

DAR ES SALAAM-TANZANIA.