Mradi ‘e- Fahamu’ unavyowavusha wenye ulemavu kuziona haki na ufanisi darasani

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 01:38 PM Apr 25 2024
Mtalaamu akiwaelezea wanafunzi namna ya kuingia kwenye tovuti ya e-Fahamu katika moja ya shule zinazofaidika na mradi huo, unaotekelezwa na Vodacom Tanzania Foundation.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mtalaamu akiwaelezea wanafunzi namna ya kuingia kwenye tovuti ya e-Fahamu katika moja ya shule zinazofaidika na mradi huo, unaotekelezwa na Vodacom Tanzania Foundation.

ELlMU kwa wote, humaanisha namna ya kuhakikisha watoto wahitaji wanapata haki zao za elimu, bila kujali tabaka zao. Kuna mfano hai, wanapojumuishwa watoto wenye ulemavu shuleni, ambao wamekuwa wakitengwa kutokana na hali zao.

Hapo kunamaanisha wanapewa fursa sawa ya kwenda shuleni kushirikiana na wenzao, kujifunza na kuendeleza stadi wanazopenda kwa maisha yao ya baadaye. 

 Ni hali inayojidhihirisha kama ambavyo shule za sekondari kadhaa zinavyotumia maudhui ya kidijitali yanayotolewa na sekta binafsi, zikipigania fursa sawa kwa wote katika elimu, afya na uwezeshaji kiuchumi. 

 Hatua mojawapo ni pale, taasisi ya Vodacom kupitia tawi lake la CSR, Vodacom Tanzania Foundation, imekuwa ikifanya miradi ya elimu ya kidijitali tangu mwaka 2017. 

 Ni katika mwaka huo ambao kupitia taasisi yake, ilianzisha tovuti ya kujifunza mtandaoni, inayojulikana kama ‘e-Fahamu’, inayotoa maudhui ya kujifunzia na kufundishia kidijitali kwa wanafunzi na walimu.

 Hivi karibuni, iliweka maabara kamili ya ICT kwenye Shule ya Sekondari ya Buhongwa iliyopo wilaya ya Nyamagana, Mwanza. Kimsingi, ni maabara iliyoanzishwa kama sehemu ya mpango mkubwa wa kuanzisha shule za mfano za ‘e-Fahamu’ nchini. 

 Maria Selestine, mwanafunzi mwenye ualbino katika Shule ya Sekondari ya Buhongwa huko Nyamagana, Mwanza, anasimulia: "Nilikuwa napata changamoto kubwa, kwa sababu maktaba yetu haina vitabu vya kutosha na shule ina wanafunzi wengi. 

“Sikuweza kugombania vitabu maktaba, lakini sasa kupitia e-Fahamu, naweza kupata chochote mtandaoni na kupata maelezo kuhusu karibu kila kitu."

Upatikanaji wa teknolojia ya kidijitali na mtandao wa intaneti bado ni changamoto katika maeneo mengi ya Tanzania, hasa vijijini. Katika kupunguza pengo hilo la kidijitali, inatajwa ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa sawa za kupata rasilimali za elimu na kukuza stadi za kidigitali. 

 Mwaka huu inatajwa programu hiyo ya e-Fahamu iliwasilisha maudhui kuhusu stadi za kidijitali, ikiwafundisha wanafunzi jinsi ya kutumia mtandao kwa usalama na maadili, pamoja na namna ya kutumia mitandao za utafutaji kama ‘Google’ kwa ufanisi wanapokuwa mtandaoni.

 Mtesigwa Bulenga, nio Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Buhongwa, anafafanua uzoefu wake kuwa"shule hii ina mfumo wa elimu jumuishi ambayo inawakusanya pamoja wanafunzi wote wenye mahitaji maalum. Tunao wanafunzi wengi, kwa hivyo maendeleo haya ya kiteknolojia yanarahisisha mchakato wa kufundisha."

 Hiyo ‘e-Fahamu’ inaangukia utambulisho ni tovuti inayorahisisha upatikanaji maudhui ya kujifunza sana, vilevile kuhudhria katika namna sahihi darasani. 

 Vilevile, inatajwa walimu wao wananufaika na zana za kufundishi, zinazoboresha uwasilishaji wao wa masomo kutoka kwenye maudhui wanayonuia darasani.

 natolewa mfano kwamba, e-Fahamu ina chaneli ya maudhui inayomuonesha mwalimu namna ya kujiandaa na somo kabla hajaenda darasani, huku wanafunzi wakitumia maudhui yanayotolewa na chaneli iitwayo het inayotoa maudhui ya masomo ya hisabati na sayansi kwa njia ya kibunifu. 

 "Hii programu (e-Fahamu) imenifanya niweze kusoma na kuelewa navyojisomea tofauti na hapo awali, nilipokuwa nategemea mkalimani kuelewa walimu walipokuwa wakifundisha darasani," anasema Zanura Rajabu, mwanafunzi mwenye ulemavu wa kusikia katika Shule ya Sekondari Buhongwa.

 Namna ya utendaji wa taasisi Vodacom, imekuwa ikiwekeza katika miundombinu, hali kadhalika kuwa mstari wa mbele kuunga mkono elimu zaidi katika maeneo ya teknolijia ya habari na mawasiliano (Tehama) na mambo ya fedha katika shule za umma. 

 Lengo hapo linatajwa, ni kuhakikisha matumizi hayo ya Tehama yanazingatiwa katiika elimu nchini, ili wanafunzi wanufaike na kufaidika kuunganishwa kimawasiliano katika ulimwengu wa kidigitali.

 Akizungumzia lengo la programu ya ‘e-Fahamu’, Zuweina Farah, Mkurugenzi wa Masuala ya Nje na Vodacom Tanzania Foundation, anasema:

 "Tukiwa kama kampuni ya teknolojia ya mawasiliano ya simu, tuna wajibu wa kutoa suluhisho la kutumia teknolojia katika elimu kwa kuwaleta wanafunzi na walimu karibu na maudhui mijini na vijijini.”

 Zuweina anaongeza kuwa "kwa maslahi ya kufanya kazi kwa pamoja kama sekta binafsi na serikali, tunalenga kuboresha matokeo ya kujifunza nchini. Lengo letu ni kuwasaidia Watanzania katika ulimwengu huu wa kidijitali na elimu ni sekta muhimu kufanikisha hili."

 Taasisi hiyo inajitambulisha katika dhamira ya kuboresha maisha ya Watanzania, ikitumia teknolojia ya mawasiliano ya simu. 

 Hadi sasa juhudi za taasisi hiyo, zinaendana kwa karibu na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hasa SDG Namba Nne, inayolenga kuwapo Elimu Bora, pia namba 10 inayolenga Kupunguza Ubaguzi, hapo mradi husika unaelezwa kuwagusa wenye ulemavu.