Narudi kwetu babu we, sikuzaliwa juu ya miti

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:42 PM May 05 2024
Mwanamke akimchoka mwanaume, utaomba ardhi ipasuke.
PICHA: MAKTABA
Mwanamke akimchoka mwanaume, utaomba ardhi ipasuke.

SIKU zote mwanamke akichoka huwa kiumbe tofauti na inavyofikiriwa. Mwanamke akimchoka mwanaume, utaomba ardhi ipasuke uingie.

Hata kama uliishi naye miaka 10, ile siku akisema kuanzia sasa hataki kuishi na wewe anaondoka ujue anamaanisha. Na akichoka ujue ni kweli maji yamemfika shingoni, amevumilia kila aina ya mateso na tabu, lakini ameshindwa kuendelea kumvumilia mwanaume.

Inaaminika kuwa wanawake ni viumbe wapole, na wavumilivu, wenye upendo, Mwanamke ndiye kiumbe pekee anayeweza kuishi na mwanaume mwenye mapungufu mengi kama ulevi, kupiga, gubu, uchoyo na vingine vingi vinavyofanana na hivyo, ambavyo kwa hali ya kawaida mwanaume asingeweza.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanaume huwachukulia poa. Na hata akimkosea, huomba msamaha na mwanamke akakubali. Wanawake ni wepesi pia kukubali msamaha wa mwanaume kuliko wenzao.

Kitu ambacho wanaume hawajagundua ni kwamba huwa wanahesabu. Mwanamke anaweka kumbukumbu kwa kila anachofanyiwa na kukiweka moyoni.

Kinachotakiwa hapo sasa usimvuruge, ukiendelea kufanya makosa ya mara kwa mara ya kujirudia, ipo siku isiyo na jina utapata unachokihitaji. Hutoamini macho na masikio yako kuona yule yule mkeo ambaye alikuwa anakutii, anabeba mapungufu yako yote, anakubali misamaha ya makosa mbalimbali mfululizo uliyomfanyia, amebadilika na sasa anachotaka ni kitu kimoja tu, muachane, umpe talaka yake aondoke. Na akishafikia hapo siku zote huwa hawarudi nyuma.

Ndiyo maana ukisoma Biblia, Waraka kwa Kwanza wa Petro 3:7, inasema hivi: 
 "Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."

Hii ina maana kubwa na moja ambayo nitaisema hapa ni kwamba wanaume hawatakiwi kuishi na wake zao kimazoea. Mke ni lazima apendwe, ajaliwe, atunzwe na kulindwa. 

Chochote mbali na hicho ipo siku unakuja kulia na kuomba siku zirudishwe nyuma ili umpe upendo uliokuwa haumpatii, pale atakapokuwa anakusaka kilicho chake na kuondoka.

Tena wanawake wa siku hizi siyo kama wale wa zamani, ambao hawaondoki mpaka umpe talaka, au mrudishwe kwa wazazi wake.

Wa kizazi cha sasa ananyanyua virago vyake, huyooo, kwa wazazi wake, anakwambia kabisa talaka itanifuata nyuma.

Ndugu yangu, hata kama huyo mke akirejea kwako, utakuwa umepoteza muda mwingi na gharama kubwa. Kikubwa hapa nawasihi wanaume vyema na wake zao au hata wapenzi wao.

Marijani Rajab aliyaona haya yametamalaki kwenye jamii na kutunga wimbo aliouita, 'Ndoa ya Mateso.'

Ni wimbo ambao unamzungumzia mama mmoja aliyechoshwa na manyanyaso na mumewe na akenda kwa mjumbe kuomba ushauri, ikiwemo kupewa talaka yake.

Tukio hili ni la kweli kabisa, ambalo Marijani alilishuhudia na maneno yaliyozungumzwa hapo yote yalitakwa na mama huyo mbele ya mjumbe. Mjumbe mwenyewe alikuwa  mama yake Marijani.

Marijali alikuwa akisafisha redio yake uani kwao maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam, mara akaja mwanamke kwa mjumbe na kumwelezea yote. Kwa sababu Marijani alikuwa  mwanamuziki, alivutiwa na maelezo ya mama yule, akawachukua na kuyatungia wimbo pamoja na maneno ya mjumbe ambaye ni mama yake mzazi.

kabla ya kurekodiwa, alikuwa akitaja mpaka jina la yule mama aliyemshtaki mumewe, lakini mama Marijani akamwambia mwanawe aondoe jina, na kumwambia akifanya hivyo watu wenye shida watakuwa wanaogopa kuja nyumbani kushtaki kwa kuogopa kutajwa redioni. Marijani akafanya hivyo, na hata uliporekodiwa haikuwa na jina la mama huyo. Mashairi ya wimbo huo ni huu hapa;- 

"Niulizieni enyi walimwengu, huyu mwanaumume anavyonitesa, hii ndiyo haki au ni mateso, hii ndiyo haki au ni mateso? Kanitoa kwetu kwa baba na mama, kwa vigelegele na heshima nyingi, tizameni sasa anavyonigeuka, tizameni sasa anavyonigeuka.

 â€œAnanipa mateso huku ugenini, sina hata ndugu wa kunisaidia, na mimi n'na watoto jamani tabu gani, na mimi n'na watoto jamani tabu gani.

Kwani kuolewa ni jambo la ajabu? Au kuolewa sana na utumwa? Kama ndiyo hivyo mimi nimeshindwa, kama ndiyo hivyo mimi nimeshindwa.

“Natoa ushahidi kwako we mjumbe, mwambie huyo bwana anipe talaka yangu, nisije kuondoka ikawa mateso, nisije kuondoka ikawa maneno.

"Mambo anayoyafanya ni aibu kusema, kwa kuwa leo nina uchungu nitakueleza. Hapa unavyotuona, hatuna chochote nyumbani, mume wangu haonekani sijui yupo wapi!

Anababaishwa na anasa za mjini, mimi kanitupa na watoto hawajali. Pesa zake zote zinaishia nje, kwa makuku ya kukaanga bibi na mkate mkavu. Nimechoka mimi na mwanamume mlevi, heri anipe talaka ili nirudi kwetu. 

Sikuzaliwa juu ya miti, nikako kwetu, ninako kwetu kwa baba na mama.

"Mateso, mateso, mateso, yamezidi nachoka.

"Pole mama kwa tabu ulizozipata, lakini kwanza, usichukue hatua hiyo mama.
 Mimi na wazazi wake, tutamwita tumkanye, akirudia, mimi nitakuwa shahidi yako mama. Naona vibaya, mmeshazaa watoto, mkitengana, mtawapa tabu watoto wenu mama."
 
 Tuma meseji 0716 350534