Serikali inavyojipanga zama mpya kukabili majanga kwa staili ngeni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:44 AM May 02 2024
Behewa la treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) lililopata ajali.
Picha: Maktaba.
Behewa la treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) lililopata ajali.

MAJANGA ya moto na ajali hadi sasa, yameendelea kutesa na kusababisha vifo, huku suluhu ya kudumu bado haijapatikana.

Matukio makubwa kuungua maduka, majengo na migahawa iliyopo Kariakoo Dar es Salaam mwaka jana na kuteketea soko la Karume Dar es Salaam mwaka juzi, yanaonyesha hali tete.
 
Mengine ambayo yameshatikisa nchini na kuua, ni ajali ya ndege Precision Air, iliyotokea mwaka jana mjini Bukoba, mkoani Kagera, ikaua watu 19.
 
MV SKAGIT – 2012

Ni ajali iliyotokea miezi 10 tu, baada ya ajali nyingine MV Spice Islander. Ilikuwa Julai 18, 2012 majira ya alasiri, meli MV Skagit ilipozama eneo la Chumbe, Zanzibar ikitoka Dar es Salaam, safarini kuelekea Zanzibar na watu 290, katika mgawanyo; wafanyakazi tisa melini, abiria watu wazima 250 na watoto 31.
 
Meli ya Skagit iliua watu 81, wakiwamo Watanzania 75; Wakenya watatu; Waholanzi wawili; Mrundi mmoja.

Aidha, watu 212 walipotea ajalini na 154 walinusurika, wakiwamo; Waholanzi watano; Wajerumani wanne; Wabelgiji, Wamarekani, na Waisraeli, idadi yao  wawili kwa kila utaifa. 
 
TRENI MSAGATI – 2002
 
Nayo inaingia katika rekodi ya ajali mbaya za reli nchini, ikitokea kilomita 388 kati ya stesheni za Igandu na Msagali, Dodoma Juni 24, 2002 saa 2.30 asubuhi, watu 281 walipoteza maisha.

Maiti 193 zilitambuliwa na kuchukuliwa, huku 88 walizikwa na mamlaka za serikali kwenye maziko iliyogusa halaiki katika makaburi ya Maili Mbili, Miyuji jijini Dodoma, Juni 27, 2002 kutokana na kutotambuliwa.
 
MV Nyerere - 2018

Mnamo Septemba 2018, watu 224 walifariki na wengine 41 wakiokolewa, katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere, mkoani Mwanza.
 
Ilikuwa ajali inayoacha kumbukumbu inayofanana na MV Bukoba iliyotokea Ziwa Victoria, Mhandisi Alphonce Charahani, akiwa wa mwisho kuokolewa, akiwa hai, baada ya kukaa majini kwa saa 48.
 
Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli akaeleza kivuko cha MV Nyerere, kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 101, lakini kwa takwimu za miili iliyopatikana, pia manusura ni wazi chombo hicho kilibeba abiria wengi kuliko uwezo wake.  
 
MV BUKOBA - 1996
Inabaki kuwa ajali ya kihistoria iliyoua watu wengi zaidi kwa wakati mmoja nchini, katika miongo ya hivi karibuni. Ilitokea Mei 21, 1996, hata serikali ikakiri ajali hiyo itaendelea kuwa kumbukumbu mbaya kitaifa ya kuangamiza maisha ya mamia ya Watanzania kwa wakati mmoja.
 
Inakadiriwa zaidi ya watu 800 walifariki katika ajali hiyo iliyotokea kilomita 56 kutoka bandarini Mwanza.
 
Imepita miaka 26 sasa tangu kuzama MV Bukoba, lakini kwa aliyekuwepo na asiyekuwapo, historia inaendelea kudumu kwao.
 
 
MV SPICE ISLANDER 
 
Kuzama meli MV Spice Islander, Septemba 10, 2011 eneo la Nungwi, Kaskazini mwa Unguja, kulileta huzuni kwa wakawzi wa mahali hapo, kukiwapo idadi kubwa ya waliofariki.
 
Ripoti ya jopo lililoundwa kuchunguza ajali hiyo, chini ya Jaji Abdulhakim Ameir, aliyewaongoza watu 10, inataja watu 1370 walipoteza maisha.

Matokeo ya uchunguzi yanaeleza, meli  ilibeba abiria idadi mara nne zaidi ya uwezo wake; ilikuwa na abiria 2,470 wakati uwezo wake ilikuwa watu 620. Ni mkasa kama huo, ndio uliipata meli MV Bukoba.
 
Tume iliyoundwa, inasema meli hiyo ilibainika kuwa na hitilafu iliyojulikana miezi miwili kabla ya kuzama,  kupitia ukaguzi uliofanywa na Taasisi ya Usalama wa Bahari, lakini bado meli hiyo ilipewa leseni. 
 
FUNZO LA MAJANGA
 
Pamoja na kupatikana majanga mengi, inalalamikiwa bado hakuna mkakati madhubuti wa kujikinga na kujiandaa kukabiliana nayo, kama inavyotakiwa na kanuni rasmi za usafiri huo.
 
Mahitaji yanayotajwa ni kuwapo Jeshi la Zimamoto  na Uokoaji lenye uwezo, ikiwa na askari wengi, wenye vifaa vya kutoha kwa uokoaji.
 
Pia, kunakuwapo vikundi vya uokoaji mbalimbali vilivyoanzishwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, vinavyopewa  mafunzo mahsusim, ili kukitokea janga, navyo vishiriki kikamilifu.
 
Hao ni wananchi vya kujitolea wanaozisaidia sana nchi zao, mfano hai Ujerumani na Japan, wanakosaidia majanga kama ya tetemeko la ardhi, ajali za barabarani, mafuriko na majanga ya moto.
 
DARASA LA UJERUMANI 
Ni kawaida kuwaona wananchi wanaojitolea nchini Ujerumani, katika operesheni zote za ukoaji wa majanga. Hao ni waliopewa mafunzo maalumu ya uokoaji, wakilipwa  wanalipwa na wanasaidia kupunguza madhara ya majanga.

Makundi hayo ya wanachi ya uokoaji, yanatajwa kusaidia hasa maeneo ya vijijini, ambako wana- Zimamoto hawana ofisi.
Kwa mujibu wa takwimu tangu mwaka 2018, kuna watu 22,000 wanaofanya kazi ya kujitolea ya uokoaji wanaolipwa, kila wanapofanya kazi hiyo tu.

MAONI NCHINI

Juma Waziri, ni mfanyabiashara wa Kariakoo, anayesimulia mkasa, kwamba duka lake liliungua moto nchini, hivyo anashauri kupitia uzoefu wake, ni busara wananchi washirikishwe kupewa mafunzo ya kujikinga na kujiokoa, pale janga linapotokea.

Anasema, wananchi wanapopewa mafunzo na kushirikishwa kuokoa, kunasaidia, badala ya ilivyo sasa wanasubiri wahusika wa Zimamoto kufika, moto unakuwa umeshateketeza mali.

Mwenyekiti wa zamani wa chama NCCR-Mageuzi, James Mbatia, anautaja moto ni miongoni mwa majanga endelevu katika maisha ya kila siku, hivyo kunahitajika elimu stahiki ya kupambana nayo, pia majanga mengine kama hayo.

Mbatia ambaye ana taaluma ya Uhandisi Ujenzi- Mazingira, anasisitiza kunahitajika utekelezaji sheria zinazosimamia majanga, kuwalinda wafanyabiashara na majanga ya moto.

“Kwa kuwa sheria ya kuanzisha taasisi ya kupambana na kusimamia majanga ipo iliyotungwa 2015 (Disaster Management Act), serikali inabidi iipe kipaumbele utekelezaji sheria hiyo, kwa kuanzisha  taasisi hiyo ya kupambana na majanga,” anasema.

WAZIRI MASAUNI

Ni tamko lake Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, kwamba serikali inadhamiria kuboresha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kwa ununuzi wa nyenzo mpya.

Hapo anazitaja kuwa; magari ya kuzima moto takriban 150, magari 20 ya kubeba wagonjwa, boti za kisasa 25 za na helikopta moja, zote ni maalumu za uokoaji.
 
Masauni akizungumza katika Mkutano wa Kuwajengea Uwezo Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala, ulioandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anataja kuwa sehemu ya juhudi za kupambana na athari za majanga, pindi zinapotokea, ikiwamo moto.

Hapo akawaomba wakuu wa mikoa kuhakikisha kunakuwapo vituo vya kuchota maji, yatakayotumika penye majanga ya moto.
 
Mengine anayataja kuwa vipaumbele kwa Jeshi hilo, ni kuimarisha vitendea kazi vya zimamoto na uokoaji, ujenzi wa vituo vya zimamoto pamoja na nyumba za makazi ya askari wa jeshi hilo.
 
Hayo yanatokea kitaifa,ipo mifano mibaya ya moto, mwaka 1994, zaidi ya wanafunzi 40 nchini, wakapoteza maisha na mali zao. 
 
Pia, mwaka 2009 shule ya sekondari mkoani ikateketea kwa moto, ikiripotiwa zaidi ya wanafunzi 20 waliripotiwa kupoteza maisha.