UNASABA WA SAMIA NA AFYA... Amewekeza mabilioni kwa rasilimali afya, akisogelea kufadhili tiba watoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:22 PM Apr 25 2024
Waziri  wa Afya, Ummy Mwalimu akikagua tiba ya watoto wenye vichwa vikubwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dar es Salaam, siku chache zilizopita, ambako akatangaza ufadhili wa tiba kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha: Maktaba
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akikagua tiba ya watoto wenye vichwa vikubwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dar es Salaam, siku chache zilizopita, ambako akatangaza ufadhili wa tiba kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

KATIKA historia ya afya inayosifiwa leo kiserikali Awamu ya Sita, inashika sura kadhaa. Mwanzo wake una mzizi wa kasi ya upanuzi ulioanzia katika awamu tatu za serikali zilizopita. Ni mwaka 1996, Rais Benjamin Mkapa akapitisha sheria ya kuwa na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), kuisaidia Hospitali Kuu ya Muhimbili, wakati huo.

Baadaye katika Awamu ya Nne, kukashuhudiwa maboresho yenye sura mbili za awali. Kwanza, serikali ikabuni Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM), ambayo ndio usukani wa yote yanayofanyika sasa, ikitimia miaka 16.

Kila mtaa au kitongoji kuwa na Zahanati, pia Kata kuwa na Kituo cha Afya na wilaya inakuwa na Hospitali. Kuanzia mkoa, Hospitali za kanda, hadi Muhimbili iliyopewa hadhi mpya Hospitali ya Taifa (MNH) zikawa za rufani.

Vilevile, MOI ikiongezewa jukumu la kutibu mishipa ya fahamu, eneo nyeti ambalo pia lilikuwa na mabingwa tiba wa kuhesabu.

Muasisi Rais Jakaya Kikwete, tena akabuni taasisi ya Moyo, JKCI, hali kadhalika ikashuhudiwa katika Awamu ya Tano, uhamisho makao makuu ya nchi kuwa mkoani Dodoma, kukibuniwa hospitali kubwa ya rufani.

Sura ya pili katika maendeleo hayo, ni kusambaza utitiri wa vituo vya afya, zahanati na hospitali kwa mikoa na maeneo yasiyokuwa na hospitali za rufani. 

Hapo ndipo panakozaliwa rekodi katika kipindi cha miaka mitatu sasa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kumejengwa zahanati na vituo vya afya zaidi ya 300, ‘kazi ikiendelea’ kwa kasi kubwa.

Vilevile kuna la tatu analolitenda, uwekezaji mkubwa wa vifaa na nguvu kazi ya wataalamu, kuanzia ajira na kugharamia masomo hadi ngazi ya shahada ya uzamivu kila mwaka kukuza uwezo wa nchi katika fani hiyo.

Ndani ya stadi hiyo, kuna ukaribishaji stadi na teknolojia ya tiba, hata imefika hatua Tanzania iko juu zaidi ya nchi jirani za Afrika Mashariki, sasa zinafunga safari nchini kujifunza, staili inayotumiwa na wataalamu kama wa MNH, MOI an JKCI, wanaoenda mikoani kusambaza ujuzi huo mikoani.

Mageuzi hayo yakiwa sehemu ya ajenda kuu ya Rais Dk. Samia katika maendeleo ya Watanzania, imefika hatua sekta afya nayo ina utalii, nchi inapata ugeni kunufaika na ‘utalii tiba’, huku wataalamu wake wakipata ugeni wa nje ya mipaka, nao wakisafiri kama vile nchini Malawi, kwenda kusambaza ujuzi na huduma itokanayo na ustadi wao.

ZAO LA MAFANIKIO

Moja ya mafanikio hayo sasa Rais Dk. Samia, mbali na kujenga mazingira bora ya kiutawala, amechukua sura nyingine akiwa ni mwekezaji.

Hivi sasa kukiwapo ‘kampeni vichwa vikubwa vinatibika’ baadhi ya wadau wakijitokeza, kudhamini tiba yao, wiki hii Rais Dk. Samia amejitokeza kudhamini tiba ya watoto 100.

Hadi sasa inajulikana watoto wazaliwao na tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi, linawakosesha raha wazazi wengi kutokana na kuwa na uwezo mdogo wa kugharamia matibabu ya watoto wao.

Mfano hai, ni ndani ya wiki moja sasa, imekuwa ikiripotiwa kwenye vyombo vya habari vya elektroniki, namna mama mwenye mtoto mwenye shida hiyo, mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, akilia kukwama kumtibu mwanawe, kwa kukosa uwezo tiba.

Hiyo ni picha ya wazazi wasiokuwa na uwezo wanavyopoteza watoto wao kwa kukosa fedha za kuwagharamia matibabu yao

Tatizo liko namna gani? Picha halisi iko kwa wanaotembelea hospitali kubwa kama Muhimbili- MNH, kinamama wengi wakiwa wamepakata watoto wenye matatizo hayo huku wakiwa na nyuso za kukata tamaa.

Baadhi yao huokoa watoto wao kwa kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema au taasisi zinazotoa msaada wa matibabu hayo.

Sasa, mageuzi hayo ya kiutawala, inakuwa ujumbe kwa kundi hilo, pale Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anatangaza Rais Dk. Samia atagharimia matibabu ya upasuaji kwa watoto hao 100. 

Pia, katika sura ya maendeleo ni hadithi ya ukombozi, kwani taifa linavuka mbali kutoka zama ilikuwa kama tatizo lisilotatulika, kuhamia upande linatatulika tena ndani ya mipaka ya nchi.

Vilevile, hilo linafanyika likiacha ujumbe mkubwa kuwapo mwanamama wa kwanza kongoza nchi na wakati huohuo, akisimamia ‘umama’ wake kutambua na kutatua matatizo ya watoto ndani ya wasifu ‘mama na mtoto huwa hawatenganishwi.’

Pia, anayetangaza kuwajibika huko anabaki ‘waziri jembe’ hasa wa afya nchini, mwanamama mwanasheria, aliyejivika viatu vya afya na vikamtosha.

Ni mara nyingine inamrudishia wasifu waziri mwenye dhamana, kwamba ‘Rais hakukosea kumteua kwa nafasi hiyo.’

Mbali na ufadhili, pia kukua stadi za tiba katika eneo hilo na mengine kama ilivyokuwa katika kampeni za kukabili maradhi ya fistula, leo darasa la kukabili uwezekano wa mtoto kuzaliwa na kichwa kikubwa, au kuwaondolea mabinti uwezekano kuwa saratani ya shingo ya kizazi, kampeni iko juu vilivyo.

Wajibu unaosisitizwa, ni wazazi wenye watoto wenye matatizo hayo sasa, wapelekwe hospitalini na kuachana na dhana kuwa wamelogwa na kuishia kwenda kwa waganga, wakipata maelezo ya uongo na mwishowe kuangukia athari mbaya.

Hayo yanafikiwa na Rais Dk. Samia, huku Chama cha Wazazi na Walezi wa Watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBATH), kikimuunga mkono kwa taarifa ya orodha ya watoto 200 wanaohitaji.