Haya yakitekelezwa kikamilifu sekta ya elimu italeta mageuzi

Nipashe
Published at 01:22 PM May 08 2024
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Picha: Maktaba
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, jana aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 wenye vipaumbele vitano. Katika utekelezaji wa vipaumbele hivyo, vyenye lengo la kuimarisha ubora wa elimu nchini, Waziri Mkenda aliomba Bunge kupitisha Sh. trilioni 1.96.

Vipaumbele ambavyo vimeanikwa katika makadirio hayo ili kutekelezwa ipasavyo ni pamoja na ujenzi wa shule za sekondari za ufundi 100 ambazo 20 kati ya hizo zinatarajiwa kufunguliwa mwakani na kudahili wanafunzi. Lengo la ujenzi wa shule hizo ni kutoa elimu na mafunzo ya ufundi ili kuwawezesha vijana wengi kuwa na ujuzi ambao utawasaidia kuwa na uelewa mpana wa masomo ya ufundi ambao utachangia maendeleo ya sekta zingine. 

Pia katika mwaka ujao wa fedha, serikali kupitia wizara hiyo, inatarajia kujenga  shule  mpya za amali (ufundi na ufundi stadi) katika maeneo ambayo hayana  vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi au shule ya amali ya sekondari. Pia wanafunzi 263,718 wanatarajia kudahiliwa katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi  ambapo 190,518 ni wa elimu ya ufundi na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 73,200.

Sambamba na kipaumbele hicho, alisema serikali itaongeza fursa za utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji kutoka 223,201 hadi 252,245 wakiwamo 84,500 wa mwaka wa kwanza ambao watanufaika na mikopo hiyo. 

Vipaumbele vingine, kwa mujibu wa Waziri Mkenda ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini na pia kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya  ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, kuimarisha ubora wa elimu ya  msingi, sekondari na ualimu.

Kadhalika, alisema katika mwaka ujao wa fedha, serikali itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 na matumizi ya mbinu  bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu.

Jambo lingine alilolibainisha ni kuipa nguvu Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili kusimamia kikamilifu utoaji na urejeshwaji wa mikopo pamoja na kufungua mashauri dhidi ya wale wanaokiuka utaratibu wa urejeshaji wa mikopo hiyo.

Ni dhahiri kwamba vipaumbele hivyo vinajibu maswali kuhusu ubora wa elimu nchini ambao umekuwa ukikosolewa mara kwa mara na wadau. Moja ya mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa ni mitaala ya elimu ambayo imekuwa haiendani na hali halisi ya sasa katika soko la ajira.

Wadau hao wamekuwa wakidai kuwa mitaala iliyopo imejikita katika nadharia zaidi kuliko vitendo hali ambayo inasababisha vijana wengi wanaohitimu kutoajirika katika sekta mbalimbali au kujiajiri. Katika hilo, serikali imejibu kwa kuboresha mitaala na kuanzisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali ili kuwezesha vijana wengi kuwa na ujuzi wa fani anuai utakaowasaidia kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira nchini.

Kilio kingine ambacho kimekuwapo kwa muda mrefu ni wanafunzi kukosa mikopo ya juu licha ya kuwa na sifa. Serikali inastahili pongezi kwa kuwa suala hilo limeainishwa kama moja ya vipaumbele na wanufaika wa mikopo hiyo wataongezeka katika mwaka ujao wa masomo ya elimu ya juu. 

Hata hivyo, kupanga ni jambo moja na utekelezaji ni jambo lingine. Kwa mantiki hiyo, jambo la muhimu ni wizara kutekeleza mipango kama ilivyoainishwa katika makadirio hayo na pia serikali kutoa kwa wakati fedha kwa mujibu wa bajeti kwenye sekta hiyo.