Bunge lisisahau kujadili maafa

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 05:04 PM May 08 2024
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Picha: Maktaba
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MABADILIKO ya tabianchi ni bayana au hakika. Si hadithi za kusimuliwa tena. Watu wameona kwenye televisheni, mitandao ya kijamii lakini wapo Watanzania wenzetu wakazi wa Rufiji.

Wanaoishi maeneo ya Mloka, Utete na Ikwiriri wameshuhudia mafuriko  makubwa  yaliyoumiza familia nyingi kuanzia kupoteza maisha na mali.

Ni ukweli kuwa Tanzania sasa inakuwa  eneo la kukabiliwa na mafuriko, kimbunga, tufani, dhoruba na hata jua na joto kali au baridi kali na sasa ni wakati wa kujiandaa na kuweka uhimilivu.

Bunge la Bajeti linavyoendelea Dodoma, huenda itapendeza kama  litaongeza muda na kuweka sawa masuala ya majanga kama ambavyo taifa limeshuhudia.

Ni vyema pia kutoa mafunzo na kuongeza zaidi bajeti na wataalamu wa masuala ya maafa kwa sababu kiasi miaka inavyosonga hili linakuwa janga la kitaifa.

Ikumbukwe kuwa  kiasi miaka  inavyokwenda ndivyo nchi itakavyokabiliwa na mafuriko mabaya na makubwa zaidi, kama   maporomoko ya ardhi.

Haya yameshuhudiwa yakiathiri mamia ya watu huko Hanang’ mkoani Manyara na Kawetere mkoani Mbeya.

Ni vyema Watanzania wakafahamu ukweli kuwa hakuna sehemu yoyote ya nchi yao ambayo inaweza kusema iko salama na ina kinga dhidi ya  mafuriko na maafa ya majanga ya kiasili.

Kuna kimbunga mathalani cha Hidaya ambacho kilileta upepo mkali  wiki iliyopita ambao ungeweza kuwa mkali na kasi zaidi ukaangusha miti, nguzo na nyaya za umeme, kuezua mabati na kubomoa majengo pamoja na kuua watu.

Upepo huo kama ungeambatana na mvua ni wazi kuwa matokeo yake yangekuwa ni athari zaidi, hivyo  ni wazi kuwa hali ya hewa inabadilika kila wakati na huenda inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo na kunatarajiwa kuwa athari  mbaya zaidi pia.

Ni wazi kuwa kimbunga Hidaya kimeipiga Mtwara na Mafia, kimesababisha mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makali na hatari baharini.

Mambo yote haya yameleta athari kwanza vifo na majeruhi, kuharibu makazi, mazao, kukwamisha na kutatiza shughuli za kiuchumi kuanzia uvuvi baharini , usafiri mfano kubomoka na kuharibiwa daraja la  Mto Matandu wilayani Kilwa.

Ndiyo maana ni  wakati wa Bunge kuamua namna bora ya kujihami na vimbunga kama Hidaya na  Jobo  ambavyo huathiri ufukwe wa Bahari ya Hindi na makazi katika pwani ya Tanzania kuanzia Tanga hadi Mtwara.

Serikali  lazima ichukue hatua madhubuti sasa na haraka ili kupunguza athari mbaya za athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo hayatabiriki.

Suala la elimu ni muhimu kuangaliwa ikibidi shule ziangaliwe zilizoko mtoni ikiwezekana  zifungwe kwa muda au zihamishwe  kuondoa uwezekano wa watoto kupoteza maisha wakati   mvua kubwa zinaponyesha.

Umeme ni suala la kuangaliwa zaidi tena kwa jicho pevu kwa kuwa  kimbunga  ambacho ni upepo mkali  kinaweza kuangusha miti kung'oa nguzo za umeme, kuharibu nyaya na  vifaa vyote vya  kusafirishia umeme mijini na vijijini. Janga hilo linaweza kuitumbukiza nchi katika giza kuu.

 Hilo nalo ni suala la kuangaliwa kwa sababu kimbunga hakimwachi yeyote salama, hata taasisi nyeti kama sekta ya umeme haziko salama.

Kuchukua tahadhari ni pamoja na kuhakikisha kuwa kuna mashine au mitambo ya  za kufua umeme kwa dharura,  magari, helkopta, dawa, huduma za  dharura iwe ni kuondoa vifusi barabarani  karibu kila mahali ili kupunguza athari za mafuriko mijini na vijijini pia.

Ikumbukwe kuwa uharibifu wa maafa kama hayo huwaacha watu bila makaazi na huduma muhimu kama maji, chakula na mavazi hilo nalo liangaliwe kwenye mijadala ya bunge ya kukabiliana na maafa na taifa kujiwekea mpango wa dharura wa kujihami na kuhimili.