Utamaduni wa kuvumiliana muhimu kuelekea uchaguzi

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 01:55 PM May 09 2024
Uchaguzi.
Picha: Maktaba
Uchaguzi.

VIONGOZI na wadau wa siasa, jana walikutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kitaifa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sheria za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliopangwa kufanyika Oktoba, mwakani.

Katika mkutano huo uliowakutanisha viongozi wakuu wa vyama hivyo, kikiwamo chama tawala, Chama Cha Mapinduzi  (CCM) ziiibuliwa hoja mbalimbali ambazo zilionyesha dhahiri kwamba hamkani hali si shwari kuelekea kwenye mchakato huo. Hali hiyo ilionekana kutokana na baadhi ya viongozi wakuu wa vyama, hasa wa upinzani kuwa na madukuduku ambayo yanaweza kutia doa katika safari ya kwenda kwenye matukio hayo makubwa ya kidemokrasi ndani ya nchi. 

Hofu kubwa zaidi imeonekana kwa viongozi hao kuonyesha wasiwasi wao kuhusu uwezo wa Tume Huru ya Uchaguzi katika kusimamia mchakato huo kama ambavyo sheria za uchaguzi ambazo zilipitishwa bungeni na hatimaye kutiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan zinavyobainisha.          

Licha ya kuonyesha hofu ya uwezo wa tume, viongozi hao walibainisha kuwa uchaguzi huo huenda usiwe huru na haki kutokana na mazingira ya nyuma. Bila kuuma maneno wala kupepesa macho, walidai kuwa hali hiyo pia inatokana na daftari la kudumu la wapigakura lilichezewa katika uchaguzi uliopita na pia kanuni za uchaguzi hazijawekwa bayana. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema haoni dalili za tume kwa mwaka huu na mwakani  kuwa na uwezo wa kusimamia uchaguzi ulio huru na wa haki huku Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akigusia suala la daftari la kudumu la wapigakura ambalo alidai halijakaa vizuri kutokana na yale yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. 

Pia aliweka bayana kwamba hata kanuni za uchaguzi hazijawekwa wazi. Kiongozi huyo hakuishia hapo bali alitupia lawama CCM kuwa ina maslahi na suala hilo na ndiyo inayoficha kanuni hizo na mchakato wa maboresho ya daktari la wapigakura. Wakati hofu hiyo ikitanda, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said, aliwapiga kijembe kuwa waache hofu kwa kuwa wanaweza kufa kabla ya wakati. 

Siasa za kidemokrasia kama ulivyo mchezo wowote, zina ushindani, hivyo kinachotakiwa ni kuwa na kanuni na sheria zisizo na upendeleo wa upande wowote. Msimamizi wa kanuni na sheria hizo ni Tume Huru ya Uchaguzi ambayo ndiyo msimamizi wa mchakato mzima na inapaswa kuwa huru bila kuingiliwa na mtu, kikundi wala chama chochote cha siasa.

Wahenga wanasema mtu akiumwa na nyoka hata akiona unyasi atashtuka. Hiyo ndiyo hofu ya wapinzani kwamba huenda uchaguzi huo usiwe huru na haki kutokana na historia na kumbukumbu ya mwaka 2020 ambao ulidaiwa kugubikwa na vitimbi vingi na walioshinda kudaiwa hawakushinda bali walipewa tu. 

Kwa mantiki hiyo, ni vyema mambo yote ambayo yana viashiria vya uchaguzi kuwa si huru na wa haki, yakafanyiwa kazi na kila kitu kuwekwa hadharani. Uchaguzi ni kwa mustakabali wa Watanzania wote na si kundi la watu au chama fulani cha siasa, hivyo sheria na kanuni ziwekwe wazi na mchakato mzima uendeshwe kwa misingi ya haki kama ilivyo kwenye sheria.

Pamoja na hayo, demokrasia katika namna yoyote ile imejengwa na misingi kadhaa ikiwamo kuvumiliana baina ya wadau. Kwa hiyo ni vyema kukawa na hali ya kuvumiliana na pale penye tashwishwi au wasiwasi, wahusika wahoji na kupata majibu huku wakitanguliza maslahi ya taifa.