Jitihada zaidi zinahitajika mapambano dhidi ya malaria

Nipashe
Published at 02:50 PM Apr 25 2024
Mapambano dhidi ya malaria.
PICHA: MAKTABA
Mapambano dhidi ya malaria.

LEO ni Siku ya Malaria Duniani ambayo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka tangu ilipoanzishwa na nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2007 wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Afya.

Lengo la kuadhimisha siku hii ni kuweka msisitizo katika mapambano ya ugonjwa huu hatari ambao umegharimu mamilioni ya watu duniani. Mapambano hayo dhidi ya malaria ni kuonyesha umuhimu wa uwekezaji endelevu na utashi wa kisiasa katika kukinga na kudhibiti malaria. 

Kaulimbuiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku ni “Kuongeza Nguvu Katika Mapambano Dhidi ya Malaria” ikisisitiza jitihada za pamoja kwa mataifa yote duniani katika kuzuia, kupambana na kutokomeza malaria. Kwa Tanzania, maadhimisho yatafanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Uyui, Tabora na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu. 

Wakati maadhimisho hayo yanafanyika pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanyika kwa serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi, takwimu zinaonyesha kuwa bado ni hatari hasa kwa watoto wachanga na walio chini ya miaka mitano pamoja na wajawazito.  Aidha, nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, kwa mujibu wa takwimu, ndizo zinazoathirika zaidi na malaria hivyo jitihada zaidi zinatakiwa katika kupambana na kutokomeza maradhi haya. 

Tamwinu za WHO zinabainisha kwamba mwaka 2022, kulikuwa na vifo 608 000 vilivyotokana na malaria na maambukizi mapya ya ugonjwa huo yalikuwa milioni 249. Asilimia 94 ya vifo na maambukizi hayo ilikuwa katika bara la Afrika na kwa mantiki hiyo, jitihada zaidi zinapaswa kufanywa kwa Afrika katika mapambano dhidi ya malaria. 

Kutokana na ukweli huo, nchi za Afrika kupitia jumuia za kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Uchumi kwa nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) zinapaswa kuweka moja ya ajenda za kipaumbele kwenye mikutano yao. 

Nchi hizo, ambazo ndizo waathirika wakubwa wa malaria, kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo na mashirika ya kimataifa zinapaswa pia kuweka mikakati thabiti katika kupambana na malaria ili kunusuru nguvu kazi na kuzifanya nchi ziwe na ustawi. 

Kuna kampeni mbalimbali na mikakati ambayo imefanyika katika kupambana na malaria katika ngazi mbalimbali lakini bado tatizo ni kubwa, hivyo inahitajika mikakati zaidi katika vita hivyo. Ili kufanikisha hilo, mapambano yanapaswa kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa na si kuachia wataalamu pekee. 

Katika kufanya hivyo, kila Mtanzania anapaswa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya yakiwamo kuteketeza mazalia ya mbu katika maeneo ya makazi, kutumia chandarua chenye dawa, kuwakinga watoto wachanga na walio chini ya miaka mitano pamoja na wajawazito ambao ndio walio katika hatari zaidi ya kupatwa na ugonjwa huo. 

Aidha, imekuwa ikisisitizwa kuwa mtu anapoona dalili za malaria, hana budi kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya vipimo na atakapobainika apatiwe matibabu stahiki. 

Licha ya maelekezo hayo, idadi kubwa ya Watanzania hawazingatii ndiyo maana ugonjwa huo umekuwa ukizidi kugharimu maisha ya watu huku taifa likiendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kinga na tiba.    

Ni dhahiri kwamba iwapo kila mtu atazingatia maelekezo ya wataalamu wa afya katika kujikinga na malaria, kutakuwa na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo na hatimaye kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi wala vifo vitokanavyo na malaria. 

Shime kila Mtanzania asimame katika nafasi yake huku akisema Tanzania, Afrika na dunia bila malaria inawezekana. Hapo ndipo ushindi dhidi ya maradhi haya utakapopatikana na hatimaye maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kuonekana.