Maboresho viwanja Ligi Kuu yaende sambamba na usajili

Nipashe
Published at 11:11 AM May 04 2024
Uwanja wa kwa mkapa.
Picha: Maktaba
Uwanja wa kwa mkapa.

WAKATI msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2023/204 unaelekea ukingoni, tayari klabu zimeshaanza maandalizi mengine kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano.

Kwa mujibu wa kalenda iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB), iliyopewa baraka na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kumalizika ifikapo Mei 28, mwaka huu.

Timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo inayodhaminiwa na Benki ya Biashara ya Taifa (NBC), zitashuka katika viwanja nane tofauti nchini kucheza mechi za kufunga pazia.

Huku tayari Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wakionekana wako katika nafasi nzuri ya kutetea taji wanalolishikilia, lolote linaweza kutokea kwa timu ambazo ziko katika hatari ya kushuka daraja, hii inatokana na kuwapo kwa tofauti ndogo ya pointi.

Timu nne kati ya saba ambazo ziko katika nafasi za chini kwenye msimamo, zinaweza kukutaka na janga hilo endapo hazitacheza vyema karata zake kwenye michezo iliyobakia ya lala salama, ikiwamo Mtibwa Sugar ambayo kwa sasa inaburuza mkia.

Kama ilivyo desturi, kila timu inafanya maandalizi yake kulingana na uwezo pamoja na kutaka kufikia malengo ya klabu husika.

Ni vizuri timu kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao pamoja na kuongeza nguvu katika mabenchi ya ufundi, wakidhamiria kusaka matokeo chanya kwenye mechi za mashindano yote wanayoshiriki.

Kumekuwa na mazoea ya timu kusahau kutengeneza au kufanya maboresho ya viwanja ambavyo wanatarajia kuvitumia katika msimu mpya na kupelekea kubadilisha vituo kutokana na viwanja walivyotarajia kufungiwa kwa sababu ya kutokuwa na hadhi ya kuchezewa mechi za Ligi Kuu.

Lakini kufungiwa au kutokuwa katika ubora unaotakiwa, timu hupelekea  kuhamahama viwanja jambo ambalo hupoteza maana ya faida ya kucheza nyumbani na kulazimika kuhamia kwenye mkoa ambao hauna timu ya Ligi Kuu kwa wakati huo.

Viongozi wa timu mtanakiwa kuhakikisha mnatengeneza viwanja ambavyo vitakuwa rafiki kwa wachezaji wengi kucheza na hatimaye kupata matokeo chanya na kuacha tabia ya kuhamahama ambayo imeonekana katika miaka ya hivi karibuni ambapo baadhi ya timu zimetumia zaidi ya viwanja vitatu ndani ya msimu mmoja.

Pia maandalizi hayo yanazihusu timu zitakazoshiriki Ligi ya Championship, hii itawasaidia kuwapa heshima wanachama na mashabiki wenu kujipanga vizuri na kujitokeza kwa wingi katika kila mechi wanayocheza badala ya kuwashtukiza kulingana na aina ya mpinzani unayekutana naye.

Kama timu zinazoitwa ndogo huko Ulaya zimekuwa zikiweka miundo mbinu mizuri, basi si vibaya na timu za hapa nyumbani zikawa na utaratibu huo wa kuboresha viwanja vyake na kuacha kubagua 'kukopi' baadhi ya mambo mazuri kutoka kwa klabu hizo zilizoko kwenye mataifa yaliyoendelea.

Lakini pia umefika wakati TFF na Kamati ya Leseni kuacha kutoa leseni kwa viwanja ambavyo havina sifa ya kutumika katika Ligi Kuu au Ligi ya Championship, ambazo hurushwa mubashara, kwa sababu ya kuendelea kuzipa heshima na hadhi zake ligi hizo.

Kwa hatua ambayo Ligi Kuu Tanzania Bara imefikia, si busara TFF kutoa leseni kwa viwanja ambavyo havina ubora na kufanya hivyo ni kuruhusu 'siasa' za nje kutawala katika soka letu.