Viongozi Simba msirudie kosa la kusajili kabla ya kuleta kocha

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:53 AM Apr 29 2024
 Kocha Abdelhak Benchikha na wasaidizi wake.
PICHA: SIMBA SC
Kocha Abdelhak Benchikha na wasaidizi wake.

TAYARI Kocha Abdelhak Benchikha na wasaidizi wake wawili, Kamal Boujnane na Farid Zemit wameachana na Simba, pia taarifa ya klabu hiyo zinaeleza kuwa mechi zilizosalia zinatarajiwa kusimamiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu hiyo, Juma Mgunda pamoja na Kocha Msaidizi, Selemani Matola.

Kuondoka kwa Benchikha si jambo la ajabu kwenye maisha ya sasa ya soka la kulipwa, kocha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Klabu zote duniani, ikiwamo Simba zimepitiwa na makocha wengi, baadhi wakiwa maarufu na wenye viwango vya juu, lakini baadaye waliondoka.

Wanaokaa milele kwenye klabu ni wanachama na mashabiki tu, lakini waliobaki, kuanzia makocha, wachezaji na viongozi huja na kuondoka.

Kwa maana hiyo kuondoka kwa Benchikha ambapo taarifa zinasema kuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyeomba hakutakuwa na athari sana kwa upande wa klabu kama viongozi watatekeleza kile ambacho baadhi ya mashabiki wanakitaka, nacho ni kuleta kocha mwingine mapema kabla ya usajili wa msimu ujao kuanza.

Moja ya sababu kubwa ya Simba kutokuwa na usajili mzuri kwa miaka ya hivi karibuni ni kuchukua wachezaji wakati timu haina kocha.

Sina kumbukumbu nzuri ya nyuma sana, lakini tangu ujio wa Zoran Maki, alikuta wachezaji wamesajiliwa na wengine wanaendelea kusajiliwa.

Hakukaa sana, akaja Roberto Oliveira, ambaye aliendelea na waliopo na hata msimu ulipoisha, ikaonekana kabisa hakushirikishwa kwenye usajili kutokana labda ya upole wake, badala yake aliletewa tu kundi la wachezaji asiwafahamu vema.

Benchikha naye amekuja katikati ya ligi akiwa amekuta wachezaji ambao haihitaji kwenda kusomea ukocha kujua kuwa baadhi wametumika sana, wamechanganyikana na wenye umri mkubwa, unajumlisha na wale ambao hawana viwango vya kuchezea timu kama hiyo, hapo utapata timu ambayo inakwenda tu, Mungu nisaidie.

Viongozi wa Simba ndiyo wamekuwa wanasajili wachezaji na makocha wamekuwa wakija wanakuta lundo la wachezaji ambao baadhi yao wanawakataa wakisema hawako kwenye viwango vya kuichezea klabu kama hiyo.

Sijajua ni bahati mbaya au makusudi miaka ya hivi karibuni, Simba inamaliza msimu ikiwa haina kocha na viongozi wanaanza kufanya usajili usio wa malengo na ufundi wowote, badala yake wanasajili timu isiyokuwa na uwiano, wachezaji wengi kwenye nafasi moja, nafasi zingine zikikosa watu imara, ikiwamo namba sita ambayo inawasumbua sana kwenye usajili kila msimu.

Kama Benchikha anaondoka, basi haraka viongozi wa klabu hiyo wanatakiwa kutafuta kocha kabla hata ya msimu kumalizika ili ahusike na usajili wa msimu ujao, vinginevyo yatajirudia yale yale ya misimu yote.

Nakumbuka Simba iliyokuwa na Patrick Aussems na  Sven Ludwig Vandenbroeck ambao walikuja mapema na kufanya usajili, walitengeneza timu imara ambayo makocha wengi waliokuja baada ya hapo hawakupata tabu, walitembelea nyota zao,  kwani waliwakuta wachezaji bora na wenye viwango vya juu kutokana na usajili walioufanya.

Na kwa sababu timu ya Simba inatakiwa itengeneze kikosi kipya na imara msimu ujao, inatakiwa iwe na kocha tayari ambaye anatakiwa angalau aje aone hata mechi mbili ili ajue pakuanzia kwenye usajili.

Viongozi hawatowatendea haki wanachama na mashabiki wao wakiendeleza utamaduni wao ule ule wa kusajili wenyewe wanavyojua, halafu ndiyo wanaleta kocha.

Hakuna kisingizio cha mchakato kuchelewa kwani klabu inajua aina ya makocha inaowahitaji, na makocha wengi Afrika hata wale wakubwa,  kwa sasa wanataka kuifundisha timu hiyo kutokana na kuwa namba tano kwa ubora barani Afrika.