Kila la kheri watahiniwa Kidato cha Sita

Nipashe
Published at 02:45 PM May 07 2024
Wanafunzi wakifanya mitihani.
PICHA: MAKTABA
Wanafunzi wakifanya mitihani.

JANA wanafunzi wa Kidato cha Sita, wameanza mitihani yao na matarajio ya wengi wakiwamo wazazi wao ni kuona wanafanya vizuri ili waweze kupata alama nzuri na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya juu.

Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), lilitangaza kuanza kwa mitihani hiyo ambayo ilianza jana na kutarajiwa kumalizika Mei 24.

Ni matumaini ya wazazi wengi kuwa watahiniwa hao wamejiandaa vizuri ni mitihani ili kuepuka aibu ambayo imejitokeza miaka ya nyuma yakuandika mambo yasiyofaa.

Mitihani ni kipimo cha wanafunzi kuona yale waliyofundishwa na walimu wao yamewaingia vizuri ili hata wanapochaguliwa kwenye kujiunga na elimu ya juu au vyuo vingine sawa na hivyo wanafanya vizuri.

Kwa mujibu wa NECTA wahiniwa 113,504, wamesajiliwa kufanya mitihani ya kidato cha sita mwaka huu na kati yao watahimiwa 104,449 ni wa shule na 9,055 ni wa kujitegemea.

Idadi ya watahiniwa ni kubwa na kila mmoja anatarajia anapomaliza apate alama nzuri ili aweze kujiunga na elimu ya juu.

Elimu ndio msingi wa maisha, bila kuwa na elimu nzuri baadhi ya mambo yanakwama kwa sababu ya kukosa mwongozo mzuri.

Tanzania kwa sasa ina vyuo vingi vya elimu ya juu hali inayowawezesha watahiniwa wengi kupata fursa ya kujiunga navyo.

Tofauti ni miaka ya nyuma, chuo kilichokuwa kikitegemewa sana ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho ni chuo cha serikali, lakini kwa sasa kuna vyuo vingi vya elimu ya juu kwenye baadhi ya mikoa.

Mbali na vyuo hivyo, pia kuna vyuo vya ufundi ambavyo vimewasaidia wanafunzi wengi wanaosoma kwenye vyuo kutoka wakiwa na utalaamu na kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira za serikalini.

Vyuo vimewasaidia wanafunzi wengi kujiendesha kimaisha kutokana na kupata elimu nzuri ya kuwasimamia wanapoanza jambo lolote linalohusu kujiajiri.

Sasa kuna wanafunzi wengi waliomaliza vyuo vya elimu ya juu ambao walisomea fani nyingine, lakini baada ya kukosa ajira serikalini, wameamua kuanzisha biashara zao na mambo yao yamekwenda vizuri baada ya kupata mwongozo.

Tofauti na miaka ya nyuma hivi sasa vijana wengi wanachakarika kujiajiri wenyewe na wengine kufanikiwa kufanya vizuri na kuajiri wenzao.

Hata Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akitoa salamu kwa watahiniwa hao amesema anatarajia kuona vipwa, juhudi na kujituma ili kuleta mchango wao katika maendeleo ya nchi siku zijazo.

Aliwaahidi kuwa ataendelea kufanyakazi, kupanga na kutekeleza mipango na sera zitakazowawezesha kutumiza nia ya kuwa na wananchi wenye mchango mkubwa kwa jamii na taifa.

Amewaahidi kuongeza fungu kwa wanafunzi zaidi kupata mikopo ya elimu ya juu na kuboresha sera na mazingira ya kukua kwa sekta binafsi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha ajira nchini.

Amewaombea watahiniwa kwa Mwenyezi Mungu wafanikishe katika hatua hiyo kwa mafanikio na kila jema katika hatua zinazofuata.

Rais wa nchi anapotumia muda wake kuwaombea watahiniwa ni jambo kubwa ambalo wanatakiwa kulichukulia kwa uzito ili wasimwangushe matokeo yanapotoka. 

Ametoa ahadi nyingi ikiwa kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Elimu, ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.