Mitihani kidato cha sita chonde chonde udanganyifu

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:53 PM May 07 2024
Wanafunzi wakifanya mitihani.
PICHA: MAKTABA
Wanafunzi wakifanya mitihani.

WANAFUNZI wa kidato cha sita, walianza mtihani wao jana, huku watahiniwa hao 13,504 wakiwamo wa ualimu ngazi ya cheti na stashahada nao wakitarajiwa kufanya mtihani wao.

Wakati wakiendelea na mitihani, si vibaya kuendelea kukumbusha kuwa vitendo vya udanganyifu ambavyo vimekuwa vikifanyika kwenye mitihani hiyo vinachangia kuporomosha elimu.

Kila mwaka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), linapotangaza matokeo ya mtihani, huwa kuna taarifa ya kuwafutia matokeo baadhi ya wanafunzi kwa sababu za kufanya udanganyifu katika mitihani hiyo.

Mfano, katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita ya mwaka 2023/2024, watahiniwa 11 walifutiwa matokeo baada ya kubainika kufanya  udanganyifu katika mtihani huo.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed. Hivyo ingekuwa ni vyema udanganyifu huo usiendelee kujitokeza katika mitihani ya mwaka huu, ili kulinda hadhi ya elimu.

Ninaamini kwamba udanganyifu wa mitihani ukidhibitiwa mitihani tutaokoa elimu yetu, kwani tabia ya wizi na udanganyifu wa mitihani limekuwa kama jambo la kawaida na kumbe elimu inakufa.

Inakufa kwa maana gani? Kwa sababu wizi ukiendelea, mwisho wake nchi itajikuta haina wasomi mahiri ambao wanafaa kuwa wataalamu bora wa fani mbalimbali hapo baadaye.

Wakati serikali ikipanga na kusimamia utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo, ni muhimu kukumbushana umuhimu wa elimu katika kuchochea maendeleo ya sekta nyingine zote.

Udanganyifu au wizi wa mitihani sio sifa njema kwa taifa kwani unachangia kuporomosha taifa kielimu, hivyo ni vyema wadau wote wa elimu kukemea na kutoshiriki vitendo hivyo.

Ni aibu kuona wanafunzi wanafaulu na kuchaguliwa kwenda katika  shule za vipaji, lakini wakifika na kufanya mitihani wakwama kupata alama za juu kutokana na kwamba walifanya wizi na udanganyifu wa mitihani.

Umefika wakati biashara ya ufaulu isiwe chachu ya wizi na udanganyifu, bali upingwe na kila mdau anayependa maendeleo ya elimu ili kuandaa wasomi bora wa baadaye watakaolisaidia taifa.

Zipo shule nyingi ambazo zinafaulisha kwa jasho na kwa mfumo wa haki, lakini pia zipo inazotumia njia ovu katika kufikia ufaulu huo ili kuvutia biashara, lakini mwisho wake ni kupata wasomi wasio na sifa.

Biashara ya ufaulu kwa njia ovu zinazotumiwa kama nyenzo au ngazi ya kumvukisha mwanafunzi kutoka daraja moja hadi jingine, kimasomo bila kujali ufahamu au uelewa wake ni hatari kwa maendeleo ya elimu.

Hivyo, kwa mchezo huu ni sawa na kuchimbia kaburi elimu yetu, taaluma ya watoto wetu na hatimaye kubakia na taifa la watu wenye ukosefu wa fikra, weledi, ujuzi na ufahamu katika mambo mbalimbali.

Katika kufanikisha vita dhidi ya vitendo hivyo, kuna haja ya kuwa na mikakati endelevu la kufuatilia hao wanaodaiwa kufanya vizuri katika mitihani ya juu ili kujua ufaulu wao tangu chini.

Njia hiyo kwa namna moja au nyingine, inaweza kusaidia kuwabaini na  hata kupata wale wanaowasaidia katika udanganyifu na kuwasaidia kupata ufaulu wa juu huku wakiwa na uwezo mdogo darasani.

Maisha ya shule ni safari ndefu yenye milima na mabonde, hivyo ni muhimu mwanafunzi ajitahidi kusoma kwa bidii ili aweze kufaulu, sio kusubiri njia mbadala ya kufaulu, yaani wizi na udanganyifu.

Niwatakie kila heri wanafunzi wa kidato cha sita walioanza mitihani yao jana, lakini wasikubali kuingizwa katika mchezo wa kuiba au kufanya udanganyifu wa aina yoyote, bali watumie uwezo wao wa darasani kulingana na jinsi walivyofundishwa na walimu wao.