TFF kuficha jina usajili tata Yanga kunazua maswali

Nipashe
Published at 11:34 AM Apr 29 2024
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini.
PICHA: MAKTABA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Aprili 12, mwaka huu, lilitoa taarifa kwa umma kupitia mtandao wake wa kijamii, likieleza kupokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), juu ya kufungiwa kwa Klabu ya Yanga kufanya usajili kutokana na kukiuka Kanuni ya Uhamisho.

TFF, ilisema uamuzi huo ulifanywa na FIFA baada ya Klabu ya Yanga kukiuka kile kilichoitwa Annexe 3 ya Kanuni ya Uhamisho (RSTP) ya shirikisho hilo. Ikasema Yanga haikuingiza uthibitisho wa malipo wa uhamishowa mchezaji husika katika usajili (TMS), licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.

Ikaelezwa kuwa klabu hiyo ilitakiwa kutekeleza matakwa ya kikanuni na kuwasilisha taarifa kwa Sekretarieti ya Nidhani ya FIFA ambapo suala hilo limefikishwa kwa ajili ya hatua zaidi.

Kwa ujumla ukisoma kwa umakini taarifa hiyo ya TFF, ina mapungufu kwani haikuandika jina la mchezaji ambaye amesababisha klabu hiyo kufungiwa kusajili kitu ambacho si cha kawaida kwa shirikisho hilo kila linapotoa taarifa hizo za Fifa.

Hatudhani hata kidogo kama FIFA haikuwaambia TFF ni mchezaji gani, hivyo ni wazi yenyewe ndiyo imeamua kuficha jina hilo na hapo ndipo wadau wa soka wanakuwa na maswali mengi ya kujiuliza ni kwa sababu gani.

Hofu hiyo inakuja kutokana na utaratibu wa TFF kuwa wa wazi kila inapotokea klabu za soka nchini kuadhibiwa FIFA.

Ni wiki iliyopita tu TFF hiyo hiyo imetoa taarifa kutoka FIFA juu ya kufungiwa kwa Klabu ya Tabora United kutokana na kumtumia mchezaji Jean Didie Touya. mbona haijaficha jina?

Huko nyuma Yanga ilikuwa na mgogoro wa wachezaji mbalimbali kama Bernard Morrison, Gael Bigirimana na aliyekuwa kocha wake, Luc Eymael, lakini haikufichwa, kila mmoja alilijua Yanga imeshtakiwa na kocha au mchezaji gani.

Hata klabu ya Simba ilikumbana na adhabu kama hiyo, ambapo TFF ilitoa taarifa yake Novemba 23, mwaka jana, juu ya klabu hiyo kufungiwa mpaka itakapotekeleza madai ya Klabu ya Teungueth ya Senegal kuhusu mchezaji Pape Sakho.

Klabu hiyo ilifungua madai dhidi ya Simba ikidai malipo ya mauzo ya mchezaji, kama walivyokubaliana kwenye mkataba wa mauziano ya Sakho, ambapo klabu hiyo ilitakiwa kuilipa timu hiyo baada ya kumpiga bei klabu ya Quevilly Rouen Metropole ya Ufaransa.

Wadau na mashabiki wa soka wanaiona TFF kama kuna kitu ambacho inakificha kwa maslahi ya Yanga, jambo ambalo tunaona ipo haja ya shirikisho hilo kuweka kila kitu hadharani ili kutoonekana linaegemea upande fulani katika maamuzi yake.

Hoja kuntu, inakuja kwa kile walichohoji kwa nini mchezaji huyo aliyesababisha Yanga kufungiwa asitajwe, badala yake kumficha? Hii inatia mashaka kwa viongozi wa TFF ambao wamejipambanua kuendesha soka bila upendeleo na ubaguzi. Nini kinalindwa hapo?

Sisi tunaamini katika uwazi, na katika hilo, TFF walipaswa wataje jina la mchezaji ili kila mdau wa soka ajue baada ya hiki nini kinaendelea na kama ni miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi za Ligi Kuu wakiwa hawajakamilisha kanuni hiyo, nini mustakabali wake?

Nipashe tunashangaa kuona hata wale wanajipambanua kama wachambuzi wa soka wakipiga kelele katika kila kinachotokea kwenye mpira wa miguu nchini, katika hili wamekuwa kimya kama wamemwagiwa maji ya baridi.

Wachambuzi ambao wamekuwa wakijadili hata tetesi za usajili, au chapisho tu la mtu binafsi, kufanya vibaya kwa baadhi ya klabu, ubora na udhaifu wa makocha mpaka uwekezaji wa klabu nchini, lakini masuala nyeti kama haya wamekuwa kimya.

Na si wachambuzi tu, pia hata viongozi wa klabu za Ligi Kuu nao wamekuwa kimya hawataki hata kuhoji kujua nini kilichopo nyuma ya pazia, hivyo tungependa kuona TFF ikiweka kila kitu hadharani ili kuondoa sintofahamu hii kwa wadau wa soka.