Benchikha adaiwa kuomba kuondoka Simba

By Saada Akida , Nipashe
Published at 12:43 PM Apr 28 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.
PICHA: SIMBA SC
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.

IMEELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha huenda msimu ujao asiwepo kwenye benchi la ufundi la Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kupata ofa ya kuinoa timu ya Taifa ya Algeria.

Taarifa za ndani ambazo bado hazijathibitishwa mapema zimesema kwamba, Benchikha tayari amewasilisha barua ya kuomba kuondoka katika Klabu hiyo.

Kwa mujibu wa tarifa hizo, Benchikha ameutaka uongozi kutoendelea kukinoa kikosi cha Simba kwa msimu ujao na kwa ajili ya kwenda kutafuta changamoto nyingine likiwemo dili hilo ambalo lipo mezani.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, uongozi umeridhia maombi yake licha ya Mwekezaji, Mohammed Dewji (Mo) kutaka kuendelea na Benchikha kwa msimu mwingine.

“Suala la Benchikha kubaki kwa msimu ujao limekuwa gumu licha ya maombi ya mwekezaji na tayari mchakato wa kupata kocha mpya umeanza mapema,” amesema mtoa habari wetu.

Ameongeza: “Msimu wa 2024/25 anakuja kocha mwingine, Benchikha anaondoka na inadaiwa kwamba anawaniwa na timu ya taifa ya Algeria,” amesema mtoa habari huyo.

Ameongeza kuwa mchakato kumpa mrithi wa Benchikha utaanza mapema ili atakapoondoka kocha huyo wawe tayari na mtu wa kumtambulisha.

Alipoulizwa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kuhusuiana na suala la Benchikha, amesema, “Sifahamu suala lolote kuhusu suala la kuondoka kwa Benchikha, ninachojua kwamba yeye ni kocha wetu, kikubwa tunapambana kuhakikisha tunashinda mechi zetu zote zilizobaki,” amesema Ahmed.

Wakati huo huo, mtoa habari huyo amesema kwa sasa mchezaji yeyote wakitaka kumsajili lazima wajumbe ambao wako kwenye kamati ya kumshauri Dewji (hawakupenda kuyataja majina yake) waende nae kwake kwa ajili ya kusaini mkataba.

Ameeleza kuwa wameanza kufanya kazi kimya kimya likiwemo suala la kocha mpya pamoja na kuwa kwenye program mpya kwa ajili ya kusaka wachezaji kwa ajili ya usajili kwa msimu ujao.