Mgunda aiongoza Simba bila nyota 6

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:45 AM Apr 30 2024
 Kocha wa Simba, Juma Mgunda.
Picha: Simba SC
Kocha wa Simba, Juma Mgunda.

WAKATI ikitangaza kuvunja mkataba na Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha pamoja na wasaidizi wake, Kamal Bounjnane na Farid Zemit, kikosi cha Simba leo kinatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi dhidi ya Namungo FC, ikiwa chini Kocha Juma Mgunda bila nyota wao sita.

Kikosi cha Simba kitashuka dimbani bila ya kuwa na Benchikha, badala yake kitakuwa chini ya Mgunda na Selemani Matola kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, ikiandikwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Imani Kajula.

Klabu hiyo na kocha Benchikha wamefikia makubaliano hayo, baada ya mwalimu mwenyewe kuomba kuvunja mkataba kutokana na matatizo ya kifamilia yanayomkabili nyumbani kwao, Algeria, ambapo yeye mwenyewe anadai anauguliwa na mkewe, hivyo anahitaji muda wa kuwa naye karibu kwa ajili ya kumuuguza. Kocha huyo raia wa Algeria alianza kukinoa kikosi hicho Novemba mwaka jana.

Hii ni mara ya pili kwa Mgunda kuteuliwa kushikilia jahazi ambapo mara ya kwanza aliteuliwa Septemba 7, 2022 na mechi yake yake kwanza ilikuwa ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi.

Kuelekea mechi ya leo, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Matola, amesema wamejipanga sawa sawa kuhakikisha wanaendeleza furaha kwa Wanasimba, huku akitaja kuwakosa jumla ya wachezaji sita kutokana na kuwa majeruhi.

"Mechi yetu na Namungo si rahisi kwa sababu wakiwa nyumbani inakuwa ni timu ngumu na hasa inapokutana na sisi, ukiacha hilo wana timu nzuri sana, wamekuwa wakipambana na hata kwenye msimamo hawapo sehemu mbaya, ila tumejizatiti na tumejiandaa.

"Mabadiliko yatakuwapo kwenye mechi ya kesho kwa sababu tuna wachezaji majeruhi wengi ambao ni,  Shomari Kapombe, Henock Inonga, Clatous Chama, Luis Miquissone, Ladack Chasambi na Sadio Kanoute naye ni majeruhi kidogo na tunamwangalia kama anaweza kucheza au la, ndiyo maana ni yeye tu peke yake tuliyekuja naye huku," alisema Matola.

Naye beki wa pembani, Israel Mwenda alisema hawataki kuwakera tena mashabiki wa Simba, hivyo wao wachezaji wamejiandaa kupambana ili kupata ushindi kwa mara nyingine tena kwenye mechi hii.

"Namungo ni wazuri, sasa kinachotakiwa ni jitihada zetu wachezaji ili kuweza kuwapiku kwa ubora kwenye kila idara, Tuko tayari, tumedhamiria kuendeleza furaha kwa Wanamsimbazi," alisema Mwenda.

Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi, alisema wanakwenda kucheza na timu kubwa ya Simba, hivyo inabidi waende kwa tahadhari na amewaandaa wachezaji wake kucheza kimkakati na kwa mfumo ambao amewaelekeza.

"Mechi itakuwa nzuri na kubwa, ukicheza na timu kubwa inabidi ucheze kwa tahadhari na kwa mikakati ili kuweza kuwazuia kwanza na baada ya hapo uwashambulie," alisema Kitambi.

Kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Novemba 9, mwaka jana, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Simba yenye pointi 46, ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, italazimika kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kwa kumaliza nafasi mbili za juu ambazo zitaifanya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, huku tishio likiwa kwa Azam FC yenye pointi 54 na Yanga inayoongoza kwa pointi 62.