Mgunda: Mechi na Azam ni kama fainali

By Saada Akida , Nipashe
Published at 08:48 AM May 08 2024
news
Picha: Mtandaoni
Kaimu Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Juma Mgunda.

KILICHOBAKI kwa Simba ni kuwania kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu, jambo ambalo Kaimu Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Juma Mgunda, amesema mechi ijayo dhidi ya Azam FC itakuwa ni kama fainali dhidi ya wapinzani wao hao.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 65, ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 57 huku Simba ikishika nafasi ya tatu kwa pointi zake 53, lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi, hivyo kama ikishinda michezo yake yote sita iliyosalia itamaliza na pointi 71. 

Kwa upande wa Azam FC ambayo itakuwa mwenyeji wa Simba kesho, ikishinda mechi zake zote tano zilizosalia itafikisha alama 72, jambo ambalo linaufanya mchezo wao huo kuwa muhimu kwa kila timu kuwania kupata matokeo chanya.

Akizungumza baada ya mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo na Tabora United juzi katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambao Simba ilishinda kwa mabao 2-0, Mgunda alikiri kuwa mechi ilikuwa ngumu hasa wanapocheza na timu ambazo ziko nafasi za chini zinazotaka kujinasua kushuka daraja.

"Kikubwa tumepata pointi tatu, wachezaji wangu wamepambana mechi ngumu, hatuwezi kudharau timu zilizopo chini ya msimamo. Hii mechi imeisha tunaenda kujipanga na mchezo ujao.

"Tunakutana na Azam FC, mchezo mgumu sana na tunaweza kusema ni fainali kwa sababu ndio unaotoa taswira ya kushika nafasi ya pili kwa sababu tunahitaji kumaliza kwenye nafasi hiyo," alisema Mgunda na kuongeza;

"Si rahisi, lakini naamini nitaisaidia Simba irudi kwenye ushindani, ninaimani wachezaji watairudisha timu sehemu nzuri, vijana waliopo wote wamepevuka na wanaelewa namna ya kufanya ili kuiweka timu katika ushindani, hivyo cha muhimu ni kuwajenga kisaikolojia na kuwarudisha kwenye morali na kila kitu kitakuwa sawa,” alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Tabora United, Masoud Djuma, alisema wamecheza na timu kubwa, na mara zote wanapokuwa nyumbani huwa wanapata faida ya nyumbani.

"Tumefanya makosa na Simba wakafanikiwa kutuadhibu, tumetengeneza nafasi tumeshindwa kuzitumia. Tunasahau matokeo hayo na tunajipanga kwa mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ili kutafuta pointi tatu, bado hatujakata tamaa tunapambana kuangalia uwezekano wa kubaki Ligi Kuu msimu ujao," alisema Masoud. 

Tabora United inashika nafasi ya pili kutoka mkiani baada ya kukusanya alama 23 katika michezo 25 iliyocheza hadi sasa, huku Mtibwa Sugar ikiburuza mkia kwa pointi zake 17 zilizotokana na kushuka dimbani mara 25.