Morocco aita Stars mpya, kuifuata Sudan Saudia leo

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 08:57 AM May 08 2024
Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman ‘Morocco’,.
Picha: Maktaba
Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman ‘Morocco’,.

KAIMU Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman ‘Morocco’, ametangaza kikosi cha wachezaji 21 wa timu hiyo watakaosafiri leo kulekea Saudi Arabia kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Sudan, huku kikiundwa na idadi kubwa ya wachezaji wapya.

Taifa Stars itacheza mchezo wao wa kwanza Mei 11 na wa pili Mei 15, mwaka huu nchini humo.

Wachezaji walioitwa katika kikosi hicho ni Makipa; Ahmed Ali Suleiman kutoka Uhamiaji FC ya Zanzibar, Ali Salum (Simba SC) na  Abrahman Vuai Nassor (U-17 TFF -TDS)

Kwa upande wa mabeki ni Mukrim Issa Abdallah (Ihefu FC), Alphonse Mabula (Msanga RFK ya Serbia), Miano Danilo (Van den Bosi - Hispania), Gadiel Michael (Cape Town- Afrika Kusini), Abdulmalik Zakaria (Namungo), Baraka Shaaban Mtui (Mashujaa FC) na Abdulrahim Seif Bausi (Uhamiaji FC - Zanzibar). 

Viougo ni Mohmed Omar Sarag  Boreham (Woog - Uingereza), Morice Michael Abrahaman  (RFK - Serbia), Khalid Habibu Iddi (Singida FG), Is-haka Said Mwinyi  (KMKM SC - Zanzibar) na Jabir Seif Mpanda (Getafe  U-17, Hispania).

Washambuliaji ni Omar Abdalla Omar (Mashujaa FC),  Ben Anthony Starkie (lIkeston Town-Uingereza), Oscar Adam Paul  (Kakamega FC - Kenya), Kelvin Pius John (KRC Genk-UbelgijI), Tarryan Allarakhia (Wealdstone Uingereza) na Ibrahim Hamad Ahmad (Zimamoto FC-Zanzibar).

Morocco alisema sababu za kuwaacha baadhi ya wachezaji wa muda mrefu wa timu hiyo ya taifa na kukabiliwa na katika klabu zao hususan mbio za ubingwa wa Ligi Kuu.

Aidha, alisema pia wapo baadhi ya wachezaji hawapati nafasi katika klabu zao ndio maana ni ngumu kujua uwezo wao kiuchezaji.

“Kuna utofauti mkubwa katika kikosi hichi kuanzia umri wa wachezaji baadhi yao wana umri mdogo, lakini pia wanauwezo mkubwa wa kiuchezaji, hivyo kama mwalimu nimeangalia vyote hivyo," alisema.

Hata hivyo, alisema anaamini wachezaji hao watafanya vizuri katika michezo hiyo miwili ya kirafiki nchini Saudi Arabia.