Nyota Stars waipa Yanga FA Cup

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 09:23 AM May 07 2024
Kikosi cha Yanga.
Picha: Yanga
Kikosi cha Yanga.

NYOTA wa zamani wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Adolph Rishard na Dua Said, wameipa nafasi kubwa Yanga kutetea ubingwa wa mashindano ya Kombe la FA ambalo kwa sasa limeingia hatua ya nusu fainali.

Yanga itacheza hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu FC, mechi itakayochezwa Mei 19, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Nusu fainali nyingine ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Benki ya CRDB itawakutanisha Azam FC na Coastal Union, mchezo utaopigwa Mei 18, mwaka huu, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akizungumza jijini jana, Rishard alisema Yanga kwa sasa iko ‘moto’ na haoni kama kuna timu inaweza kuizuia isibebe ubingwa wa michuano hiyo.

Alisema wachezaji wa Yanga wamekuwa na morali kubwa na kila anayepata nafasi ya kucheza anapambana kuonyesha kiwango bora ili kufikia malengo ya timu yao.

“Kiukweli Yanga kwa sasa wako moto, wako ‘on fire’, mimi kwa maoni yangu nawaona wakienda kubeba ubingwa wa michuano hii”, alisema nyota huyo wa zamani wa Pan African.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba, Saidi alisema Yanga iko katika ubora mkubwa na kama haitatokea vinginevyo, ubingwa wa michuano hiyo utatua klabuni kwao.

Mshambuliaji huyo alisema matokeo mazuri wanayopata Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara yamekuwa ni chachu ya kufanya vizuri pia katika michuano hiyo.

“Kwa macho yangu nawaona Yanga wakienda kushinda tena taji hili, labda itokee vingine kwa sababu katika mpira lolote linaweza kutokea,” aliongeza mshambuliaji huyo.

Fainali za mashindano hayo ambazo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, itafanyika Babati mkoani, Manyara.