Pamba FC kupokewa Mwanza kifalme leo, Ruvu, Pan zashuka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:04 AM Apr 30 2024
Wachezaji  Pamba FC wakishangilia.
Picha: Maktaba
Wachezaji Pamba FC wakishangilia.

KIKOSI cha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Pamba FC, leo kinatarajiwa kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa soka jijini Mwanza na vitongoji vyake, kikitokea jijini Arusha ambako kilifanikiwa kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya miaka 23.

Pamba, iliyotikisa kuanzia katikati ya miaka ya 1980 hadi 1990, kabla ya kuteremka daraja 1999, juzi ilifanikiwa kurejea Ligi Kuu, baada ya kuichapa Mbuni FC mabao 3-1 katika Ligi ya Championship, mechi ikichezwa, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Matokeo hayo yanaifanya Pamba kumaliza ligi hiyo ikiwa nafasi ya pili na pointi 67, ikiungana na KenGold ambayo ilikuwa ya kwanza kupanda, lakini katika mechi ya juzi pia ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, na kutwaa Ubingwa wa Championship msimu huu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi, akisema yameandaliwa mapokea ya kifalme jijini Mwanza wakati kikosi hicho kitakapowasili leo kikitokea Arusha.

"Utaratibu umeshaandaliwa, kesho (jana), tunasubiri basi letu la kisasa ambalo linaandaliwa , litakuja hapa kuwabeba vijana wetu, benchi la ufundi na viongozi kuelekea Mwanza.

Safari itaanza kesho (jana, Jumatatu), kuelekea Shinyanga, tukifika hapo tutapata mapokezi kutoka kwa mashabiki wa hapo, Jumatatu (jana) tutalala Shinyanga, Jumanne (leo) tutaondoka na mashujaa wetu, saa nne asubuhi tutapokelewa Kwimba, hapo tutakuta magari mawili yaliyoandaliwa maalum kwa ajili ya 'paredi' yameshaandaliwa kwa ajili ya kuingia katika Jiji la Mwanza," alisema Mkuu wa Mkoa huo.

Wakati Pamba ikitarajiwa kupata mapokezi makubwa, timu za Mbeya Kwanza na Biashara United zitacheza 'play off' kwa ajili ya kupata timu moja itakayocheza 'play off' ya pili na timu itakayotoka Ligi Kuu.

Mbeya Kwanza imemaliza nafasi ya tatu na pointi 65 baada ya kuichapa Transit Camp mabao 2-0, Biashara United ikikamata nafasi ya nne ikimaliza na pointi 62, kwa kuitwanga Cosmopolitan mabao 2-0.

Ligi hiyo imehitimishwa kwa timu za Ruvu Shooting na Pan African kushuka daraja, ambapo msimu ujao zitacheza Ligi Daraja la Pili, 'First League.'

Ruvu imeburuza mkia ikimaliza na pointi na 13, wakati Pan African ikimaliza nafasi ya 15 na pointi zake 20.