Yanga kumfunga Aziz Ki, hofu kwa Kagera Sugar leo

By Shufaa Lyimo ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 08:41 AM May 08 2024
news
Picha: Mtandaoni
Stephane Aziz Ki.

WAKATI ikielezwa kuwa katika hatua za mwisho za kumfunga nyota wake, Stephane Aziz Ki, kwa kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili, Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, Miguel Gamondi ameihofia Kagera Sugar, akisema mechi hiyo itakayopigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi leo itakuwa ngumu.

Taarifa zilizolifikia Nipashe jana kutoka kwa chanzo chetu ndani ya klabu hiyo, zilieleza kuwa pande zote mbili zimefikia makubaliano na kwamba kilichobaki ni Aziz Ki tu kutia saini mkataba mpya kabla ya kwenda kwao kwa mapumziko msimu huu utakapomalizika.

Mtoa habari huyo alisema wakala wa Aziz Ki ambaye ni mama yake mzazi, alikuwapo nchini kwa ajili ya kukamilisha dili lake la kuongeza mkataba na kila kitu kimeenda vizuri baada ya mchezaji huyo kukubali kusalia ndani ya kikosi cha Yanga kwa miaka miwili mingine.

“Mbali na Aziz Ki, kuna wachezaji wengine wapo kwenye mazungumzo ya kuongezewa mkataba akiwamo Shomari (Kibwana) ambaye Azam FC wanamhitaji. Wanaendelea kufanya mazungumzo na nyota ambao mikataba yao ipo ukingoni na wapo kwenye mipango ya Gamondi.

Kuhusu wachezaji wapya, wapo kwenye mazungumzo na Yusuph Kagoma wa Singida Fountain Gate FC, lakini wanazungumza na kiungo wa Simba, Clatous (Chama) ambaye bado mambo hayako sawa,” kilisema chanzo hicho.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amekiri kuwa baadhi ya nyota wao mikataba yao ipo ukingoni na wako nao katika mazungumzo akiwamo Aziz Ki na nyota wengine ambao wapo kwenye mipango ya kocha Miguel kwa msimu ujao.

“Mkataba wa Aziz Ki unafikia ukingoni na utamalizika mwishoni mwa msimu huu, ninachokijua sasa hawezi kujiunga na timu nyingine, moja ya mikakati ya Rais wa Yanga, Hersi (Saidi) ni kuhakikisha wachezaji wetu bora wanasaini mkataba mpya akiwamo Stephane,” alisema Kamwe. 

Wakati huo huo, kuelekea mchezo wao wa leo dhidi ya Kagera Sugar, Gamondi aliiambia Nipashe kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao hasa akikumbuka mechi ya kwanza ugenini walitoka sare.

Yanga inashuka dimbani ikitoka kuvuna pointi tatu katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma dhidi ya Mashujaa FC, huku Kagera Sugar ikitoka kuambulia alama moja dhidi ya KMC kutokana sare ya kutokufungana. 

Gamondi alisema amejipanga vizuri kuhakikisha anapata pointi tatu katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa. 

Alisema anatambua ugumu wa timu hiyo, hivyo amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanapambana ili wapate matokeo wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani. 

"Kwa upande wetu tumejiandaa vizuri kuelekea kwenye mchezo wetu wa kesho (leo) dhidi ya Kagera Sugar ni mchezo ambao utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa hivyo tutapambana ili tupate pointi tatu," alisema Gamondi.

Alisema kwa sasa hawazungumzii ubingwa bali anaaangalia michezo iliyopo mbele yao kwa madai kuwa iliyobaki ni migumu, jambo ambalo amewaomba mashabiki wao waendelee kuwapa ushirikiano ili washinde.

Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chamberi, alisema wataingia kwa tahadhari kubwa kwa kuwa wanakutana na timu yenye ubora wa hali ya juu msimu huu. 

"Mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa Yanga ni timu ambayo ina wachezaji wenye viwango vya hali ya juu, vile vile ipo kwenye harakati za kutangaza ubingwa," alisema Chamberi.