Yanga yanasa beki 3 wa DRC

By Saada Akida ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:02 AM May 07 2024
Chadrack Boka.
Picha: Maktaba
Chadrack Boka.

WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, akitamba kuwa dozi zitaendelea kama kawaida kwenye mechi za Ligi Kuu, licha ya kukutana na upinzani mkali kwa baadhi ya timu, klabu hiyo ipo katika hatua za mwisho kumsainisha beki Chadrack Boka kutoka Klabu ya Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Taarifa zilizopatikana jana zinaeleza kuwa Yanga ipo karibuni kupata saini ya mchezaji huyo anayecheza nafasi ya beki wa kushoto, ili kuchukua nafasi ya Joyce Lomalisa ambaye huenda akaondoka mwishoni mwa msimu, lakini ikiwa ni pendekezo la kocha Gamondi.

Mtoa taarifa huyo amesema Rais wa Yanga, Hersi Said, yupo nchini humo kwa ajili ya kusaka baadhi ya wachezaji wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao wa mashindano.

Imeelezwa kuwa Hersi pia amekutana na Rais wa Klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi kwa lengo la kuzungumza na kujadilia mambo mbalimbali ikiwamo uendeshaji wa timu, lakini na suala zima la usajili wa wachezaji.

"Siyo huyo tu, kocha ametoa mapendekezo ya wachezaji kadhaa na suala la straika ndiyo limezingatiwa zaidi maana tangu alipoondoka Mayele (Fiston), hajapatikana mtu sahihi, waliokuja bado hawajaweza kukidhi mahitaji ya safu hiyo, pia tunaendelea kuimarisha safu ya ulinzi," alisema mtoa habari huyo.

Yanga ipo katika mipango ya kuachana na baadhi ya nyota wake, ambapo mbali na Lomalisa, yupo Mahlatse Makudubela maarufu kama 'Skudu' na Bakari Mwamnyeto ambaye hataongezewa mkataba, taarifa zikisema wakala wake amemtafutia timu nchini Afrika Kusini.

Habari zinasema kumekuwa na mvutano kati ya Augustine Okrah na Kennedy Musonda nani anatakiwa kuachwa kwa ajili ya kupisha usajili wa mchezaji mwingine ili kukiimarisha kikosi hicho.

Wakati huo huo, kocha Gamondi ametamba kuwa timu yake inahitaji pointi tatu katika kila mechi ili kutwaa ubingwa, hivyo hatoangalia ukubwa au udogo wa mchezo.

Akizungumza baada ya mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo na Mashujaa FC, uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika juzi na Yanga kushinda bao 1-0, Gamondi alikiri kuwa mechi ilikuwa ngumu mno, lakini kwa sababu kila mmoja anajua kuwa wanahitaji ubingwa, ushindi ukapatikana.

"Mashujaa FC ni timu nzuri, imepambana sana, mechi ilikuwa ngumu kwetu na nimempongeza kocha wao, ila walikuwa hawajui kuwa wanacheza na timu inayohitaji matokeo zaidi kwa sasa kuliko kipindi kingine chochote.

"Kipindi cha kwanza tulikuwa na mchezo mzuri, tulimiliki mpira, tulitengeneza nafasi, tukafunga bao moja ambalo ni muhimu.

Kipindi cha pili wapinzani wetu walikuja juu, bila shaka walitaka kurudisha bao, walihitaji pointi, walipiga mipira mirefu na krosi nyingi, nadhabni walikuwa vizuri kuliko sisi, kilichoamua matokeo ni uzoefu na dhamira, ninashukuru kupata pointi tatu ugenini, hasa kwa uwanja kama huu," alisema Muargentina huyo.

Naye kocha Mohamed Abdallah 'Bares', wa Mashujaa FC aliwasifu vijana wake, akisema ni kosa moja tu ndilo lililowahukumu.

"Tumecheza vizuri, kipindi cha kwanza tulikuwa na 'plani' yetu, tulijaribu sana kuzuia, kwa sababu unajua Yanga ni timu ambayo mchezaji mmoja mmoja anaweza kuamua matokeo, kwa hiyo tuliingia na tahadhari, tukafanya kosa moja wakatuhukumu," alisema.