Zitakazopanda Ligi Kuu, 'play off', Ligi ya Championship kujulikana leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:53 PM Apr 28 2024
Wachezaji wa Pamba FC wakikabiliana na Mashujaa.
PICHA: MAKTABA
Wachezaji wa Pamba FC wakikabiliana na Mashujaa.

TIMU moja itakayoungana na Kengold kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara, na mbili zitakazocheza mechi za mchujo, 'play off', zinatarajiwa kujulikana leo, wakati wa kuhitimisha kwa Ligi ya Championship, kwenye michezo nane itakapofanyika viwanja mbalimbali nchini.

Timu ya Pamba FC, ambayo ipo katika nafasi nzuri zaidi ya kupanda Ligi Kuu, itakuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kukipiga dhidi ya Mbuni FC.

Mabingwa hao wa Ligi ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1990, wanahitaji ushindi tu kuweza kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuteremka mwishoni mwa miaka ya 1990.

Pamba ambayo ina pointi 64, inahitaji ushindi ili kufikisha pointi 67, ambazo haziwezi tena kufikiwa na timu yoyote ya chini yake, hivyo kuungana na KenGold, yenye pointi 67, huku tayari ikiwa imeshakata tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, lakini leo itahitimisha mechi yake kwa kucheza na Polisi Tanzania, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Shughuli nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, wakati Mbeya Kwanza itakapoikaribisha, Transit Camp, katika mechi ambayo inaweza kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo.

Mbeya Kwanza ambayo inashika nafasi ya tatu kwa pointi 62, kama ikishinda mechi hiyo itafikisha 65, na kama Pamba ikifungwa na kubaki na pointi zake 64, timu hiyo itakata tiketi ya kwenda Ligi Kuu.

Kama ikipata matokeo yoyote na Pamba ikishinda, basi moja kwa moja itapata nafasi ya kucheza 'play off' dhidi ya Biashara United ambayo ipo nafasi ya nne, ikiwa na pointi 59.

Mshindi wa mechi mbili za 'play off' nyumbani na ugenini, ataisubiri timu moja kutoka Ligi Kuu kwa ajili ya 'play off' nyingine, ambayo itaamua timu ya kupanda, kushuka au kubaki.

Biashara itacheza dhidi ya Cosmopolitan, Uwanja wa Karume, Musoma, Mara, TMA itakipiga na Copco, Uwanja wa Black Rhino, Karatu, Arusha, Pan African ipo Meja Jenerali Isamuhyo dhidi ya Stand United, Green Warriors, itacheza na Ruvu Shooting, Mabatini, Mlandizi, Pwani, na FGA itakipiga dhidi ya Mbeya City, Majimaji, Songea.