Bashe azibana kampuni zinazodaiwa na wakulima wa tumbaku

By Renatha Msungu , Nipashe Jumapili
Published at 01:24 PM Mar 31 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
PICHA: WIZARA YA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, ameziagiza halmashauri kushirikiana na wakuu wa mikoa kuzikamata na kuzifikisha mahakamani kampuni zinazodaiwa na wakulima wa zao la tumbaku, fedha zinazofikia Sh. bilioni nne.

Kadhalika, amemwagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, kuhakikisha vyama vinalipa fedha katika mabenki kwa sababu wakulima wameshalipa katika vyama husika.

Waziri Bashe ametoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa wadau wa tasnia ya tumbaku uliofanyika jana jijini Dodoma.

Amesema ni kosa kubwa kukaa na malipo ya wakulima ndani ya mwaka kitendo ambacho ni kuwarudisha nyuma katika kilimo wanachofanya.

Amesema anahitaji kupata taarifa ya watu kukamatwa na kuchukuliwa hatua ili kulipa madeni ya wakulima.

“Ninaziagiza halmashauri na wakuu wa mikoa hakikisheni kampuni hizo zinakamatwa na kufikishwa mahakamani,” ameagiza Bashe.

Amesema wakulima hulima mazao na kupeleka katika kampuni hizo ambazo hukaa na fedha zao kinyume na sheria, hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua.

Bashe amesema hadi kufikia Jumatano, vyama hivyo vinatakiwa viwe vimekutana na kutoa taarifa sahihi kuhusu madai yao katika benki.

Alisema anaamini wakulima wamelipa fedha hizo isipokuwa vyama ndivyo vinavyochelewesha malipo kwa wakulima.

“Kitendo hicho sio kizuri kwa kuwa, wanachelewesha maendeleo ya wakulima, kwa sababu na wao watachelewa kupata uwezeshaji kutoka katika benki.

Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku, Stanley Mnozya, alisema wakulima wanadai fedha kutoka kwa kampuni, lakini anaamini zitalipwa ili waendelee na kilimo.

Amesema lengo lao ni kuona wakulima wanapata stahiki zao ambazo zitawasaidia kupiga hatua katika kilimo ambacho wanafanya.

Akizungumzia kuhusu kilimo hivyo, amesema msimu ujao wamejipanga kuzalisha tani nyingi ili kuweza kuingia katika ushindani wa uzalishaji zao hilo.

Amesema nchi ya Zimbabwe inaongozwa katika uzalishaji, lakini wanajipanga kuhakikisha wanawafikia ama kuwapita katika uzalishaji wa zao hilo.

Awali, mkulima wa tumbaku, Hamza Rajabu, ameiomba serikali kuingilia kati madai yao ili waweze kulipwa stahiki zao wanazodai kutoka katika kampuni.