Mbunge ashangazwa kasi mikopo ya kausha damu, matumzi ya shisha

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 06:04 PM Apr 07 2024
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Cecilia Paresso.
PICHA: MAKTABA
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Cecilia Paresso.

MBUNGE wa Viti Maalum (CHADEMA), Cecilia Paresso, ameelezea kushtushwa na kasi ya matumizi ya dawa za kulevya ikiwamo shisha pamoja na mikopo inayolalamikiwa, maarufu kama ‘kausha damu’ na kuitaka serikali kutilia mkazo sheria ili kunusuru jamii.

Akichangia wakati wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/25, Paresso alisema ili taifa kuwa na maendeleo, lazima kuwapo ustawi wa jamii, watu kuwa na hali nzuri ya kiakili, kiafya na kiuchumi.

Paresso amesema kwa sasa matumizi ya shisha yamekuwa makubwa kupindukia, hususani kwa vijana wadogo ambao wanarundikana katika kumbi za starehe wakitumia kileo hicho, hali inayotengeneza wagonjwa watarajiwa wa baadaye.

“Nimesikia kwa Afrika Mashariki ni Tanzania tu bado tunatumia ‘shisha’, kwingine wamepiga marufuku. Je, sisi tunafanya nini katika hilo? Zaidi ya hapo, tunajiandaa kuja kuweka fedha nyingi katika sekta ya afya ili kuanza kutibu mzigo mkubwa wa wagonjwa wanaotokana na madhara hayo,” amesema.

Amesema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharimia matibabu ya magonjwa makubwa yasiyoambukizwa ambayo yanasababishwa na mienendo mibovu ya watu, wakiwamo vijana wanaotumia shisha na kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakitajwa kuongoza kwa kusababisha vifo Tanzania.

“Kila mara tumekuwa tukielezwa kuhusu madhara ya utumiaji wa vitu hivi hatari lakini tunafanyaje ili kuhakikisha tunadhibiti kabla havijaleta matatizo? Yawezekana ni biashara ya watu, lakini ni kwa kiwango gani na elimu inatolewa kwa kiwango gani ili mtu ajue?” amehoji.

Ameishauri serikali kuweka mkakati wa kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kudhibiti ongezeko la wakopeshaji wasiyokuwa rasmi maarufu ‘kausha damu’, ambao wamekuwa wakisababisha wananchi kufilisika.

“Iko mifuko ya kuwezesha wananchi kiuchumi zaidi ya 18, tuone namna ya kuiunganish pamoja na ile mikopo inayotolewa na halmashauri na kupata mfuko mmoja au miwili itakayoratibiwa na serikali na kutoa elimu kwa kuwafikia wananchi wa chini.

“Tuone ni namna gani tunaweza kuwasaidia kwa kuwakopesha kwa masharti nafuu na kuwanusuru na mikopo hiyo hatari, kwani wananchi hao wamekuwa wakishindwa kuzifikia benki kutokana na kuwapo kwa mashariti makubwa,” amesema.

Amesema kuna taasisi zinazotoa mikopo kisheria na kuonyesha shaka kwa baadhi kutosajiliwa na kutoa mikopo yenye athari katika jamii hadi kupewa majina tofauti kutokana na kusababisha madhira kwa wakopaji.

Mikopo hiyo, amesema huwa na riba kubwa na wakati mwingine imekuwa ikisambaratisha familia, matukio ya watu kujiua, huku wengine wakiua ndugu zao ili kupata fedha za kurejesha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika hotuba yake kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikalini na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya yake kwa mwaka 2024/25, alikiri kuwa vijana wenye umri wa miaka 30 na kuendelea wamebainika kuwa na magonjwa sugu.

Ameyataja magonjwa hayo ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari pamoja na uzito uliozidi, licha ya elimu ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kutolewa kwa zaidi ya watu 1,107 nchini.

Kuhusu ustawi wa wananchi, Majaliwa amesema serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa.

Amesema kwa kipindi cha mwaka 2023/24, kupitia programu hiyo, serikali imekamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023.

Pia amesema wanakamilisha programu mbalimbali za kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kwa lengo la kuongeza fursa za kiuchumi na kuwajengea uwezo wa mbinu za kibiashara, kupata mitaji, masoko na mikopo.

Kadhalika, amesema imeanzisha madirisha maalum ya kuwezesha wanawake kupata mikopo yenye riba nafuu ili kupunguza umaskini kwa wanawake kwa kuwawezesha kupata mitaji.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2023/24, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 1.27 ilitolewa kwa miradi 56 ya vijana.

Utafiti uliofanywa na Dk. Anna Merchetti, kutoka nchini Uswizi na kupitishwa na katika jarida la afya la ‘European Journal of Case Reports in Medicine’ mwaka 2020, umebaini matumizi ya shisha kuwa chanzo cha ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) unaoshambulia mapafu.