DC Mpogolo awafunda Mama Lishe, agawa mitungi ya gesi

By Pilly Kigome , Nipashe Jumapili
Published at 07:30 AM Mar 24 2024
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo.
Picha: Pili Kigome
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amekutanisha Mama Lishe wa wilayani hiyo kupokea kero zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ikiwemo na kuwataka waunde vikundi vya umoja ili waweze kupata fursa mbalimbali zipatikanazo nchini ili waweze kujiendeleza katika biashara zao.

Wito huo ameutoa jana jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Karimjee  wakati wa mafunzo na Maonesho ya  Mama Lishe wa wilayani hiyo.

Mpogolo amekutana na MamaLishe kutoka katika Soko ya Ilala, Machinga, Buguruni, Mchikichini, Feri, Kisutu na Kigogo Sambusa kupokea kero zinazowakabili maeneo yao ya kazi.

Mpogolo amelitaka kundi hilo kuwa na umoja na mshikano waunde makundi  ya pamoja kama ilivyo bodaboda, bajaji, wamachinga na makundi mengine ili waweze kutanua wigo wa kupata fursa.

Pia amewataka wapendane katika kazi zao na kubainisha wanawake wengi katika shughuli za utafutaji walio wengi hawapendani na kuwekeana chuki pindi anapoona mwingine anafanya biashara kwa kumzidi na kuwasisitiza upendo katika kazi ndio silaha kwani wanaweza wakainuana na hatakuombana ushauri na kubadilishana ujuzi katika harakati zao hizo.

“Niwaombe mama zangu na dada zangu  shikamaneno, pendaneni, anzisheni makundi ya umoja kama walivyo wenzenu bodaboda fursa zinawapita” amesisitiza

Wakati huohuo aligawa zawadi ya mitungi ya gesi kwa mamalishe washindi waliofanya vizuri katika kazi zao katika mashindano yaliyoshindanishwa katika baadhi ya masoko kwa vigezo vya usafi na mapishi bora.

Afisa Lishe Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,Neema Mwakasege amesema kundi hilo ni kundi muhimu sana na hivyo wanawapatia elimu ya lishe mara kwa mara kwani Watanzania wengi wa tabaka la Kati wanakula chakula kwa mama lishe.

Amesema wanawapatia elimu ya lishe ikiwemo na kuwaelimisha jinsi ya kuanda a vyakula vya makundi sita(6) ili walaji waweze kupata mlo kamili unaostahili katika mwili wa binadamu.

Vilevile wanatoa mafunzo ya kuzingatia usafi wawapo kazini kwa kufanya hivyo afya za watanzania zitabaki kuwa salama na kufafanu tayari wameshawafikia mama lishe zaidi ya 1500 katika kata 36 za Wilaya ya Ilala.

Naye Meneja wa Benki ya NMB Ilala,Christine Lifiga amewataka kundi hilo kuchangamika fursa zipatikanazo katika benki hiyo ili waweze kujiendeleza katika biashara zao za kila siku.

Amefafanua ndani ya Benki hiyo kuna mikopo mbalimbali yenye masharti nafuuu ambayo wanaweza kuchukua ili waendeleze biashara zao ukiwemo mkopo uitwao “Mshiko Fasta”  ambao unaweza kukopa kuanzia Shilingi elfu kumi hadi Milion Moja bila dhamana yoyote.

Hata hivyo baadhi ya Mamalishe kutoka katika baadhi ya Masoko waliweza kutoa kero zao akiwemo Domitia Ngwale mwakilishi kutoka soko la Mchikichini amesema changamoto kubwa inayowakabili ni kuwa sehemu yao ya kufanya biashara imewekwa karibu na dampo la takataka jambo ambalo linawakwaza kwakipindi kirefu na kumuomba Mkuu huyo kushughulikia jambo hilo.

Mwakilishi kutoka soko la Kisutu amesema changamoto inayowakabili kukosa mahala pa kumwagia maji taka na uwepo wa dampo la taka karibu na eneo hilo.