Othman alia watumishi kukosa uadilifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:00 PM Apr 07 2024
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.
PICHA: MAKTABA
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema pamoja na Zanzibar kuendelea kuhitaji wataalamu zaidi katika fani mbalimbali, bado kuna tatizo kwa baadhi ya wataalamu na wasomi kukosa uadilifu katika utumishi.

Othman ameyasema hayo baada ya futari ya pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lumumba walioko kambini kujitayarisha na mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.  

Amesema baadhi ya wasomi walioko katika utumishi, wamekuwa wakikosa uadilifu na uzalendo kwa kufanya ubadhirifu wa mali za umma pamoja na kuendekeza rushwa jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya nchi

Makamu wa kwanza wa Rais amewataka wanafunzi hao kujiandaa katika kutenda uandilifu na kuwa wazalendo wa kweli kwenye dhamana mbalimbali watakazokabidiwa na kuendelea kuitumikia vyema nchi yao. 

Kwa mujibu wa Othman, kwa kufanya hivyo, watakuwa  mfano mwema katika juhudi za pamoja za kuijenga Zanzibar na kuleta maendeleo kwa manufaa ya wananchi wote.

Amesema shule ya Lumumba ndicho kitovu cha elimu Zanzibar chenye historia kubwa katika kutoa wataalamu na wasomi wengi wa sekta mbalimbali nchini, hivyo ni alama kubwa ya elimu kwa Zanzibar na inahitaji kutunzwa.

Othman amewataka walimu na viongozi wizara kwa ujumla, kuendelea kuitendea haki alama hiyo ya elimu kwa Zanzibar kwa kuonyesha kuwapo wataalamu bora wenye madili mema kwakuwa Lumumba ndio mtambo na kiwanda muhimu cha kuzalisha wataalaamu hao.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Said, akitoa salamu baada ya futari hiyo, amesema serikali imekuwa ikichukua juhudi kubwa katika kutoa kipaumbele kwenye uwekezaji wa sekta ya elimu hasa ujenzi wa madarasa na vifaa vya kufundishia pamoja na ajira kwa walimu.

Amesema hatua hiyo imeonyesha kuwapo dalili kubwa za kupatikana mabadiliko ya kimaendeleo katika sekta ya elimu Zanzibar.

Pia amesema ufaulu wa wanafunzi wa michepuo na vipawa umeonezeka kuanzia mwaka 2021  kutoka wanafunzi 2,200 hadi  wanafunzi 6,600  kiasi ambacho ni onezeko la mara tatu la zaidi ya mafanikio jambo ambalo limechangiwa kwa kuwapo juhudi kubwa za walimu katika kuwafundisha wanafunzi wao. 

Mkuu wa Shule hiyo, Mussa Hassan, amesema ujio wa wa viongozi wakuu katika shule hiyo ni motisha kwa walimu kuendelea kuhamasika kufanya kazi kwa bidiii na pia ni deni kwa wanafunzi  kujitaidi katika masomo yao ili kuendelea kufanya vyema na kupata matokeo mazuri.

Amesema viongozi wanafahamu kwamba Lumumba ni shule iliyowekezwa sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi kielimu Zanzibar.

Naye Mwanaarabu Said Mbwana, kwa niaba ya wanafunzi wenzake, amemshukuru  Othman kwa uamuazi huo wa kufutari  nao pamoja na kuahidi kwamba watafanya kila juhudi katika masomo ili malengo yao ya kufaulu katika kiwango cha daraja la juu yafanikiwe.