TANAPA yang’ara tuzo za umahiri

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 05:16 PM Apr 07 2024
Ofisa Uhifadhi Mkuu Catherine Mbena Mkuu wa Idara ya Mawasiliano -TANAPA  (kulia) akipokea Tuzo kutoka kwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Maryprisca Mahundi Baada ya kuibuka washindi.
PICHA: TANAPA
Ofisa Uhifadhi Mkuu Catherine Mbena Mkuu wa Idara ya Mawasiliano -TANAPA (kulia) akipokea Tuzo kutoka kwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Maryprisca Mahundi Baada ya kuibuka washindi.

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Idara ya Mawasiliano limeibuka mshindi katika tuzo za Umahiri katika Mawasiliano ya Umma zilizotolewa juzi mkoani Dar es Salaam.

Tuzo hizo zilizobeba dhima ya “The Best Use of Influencers Category for the Year 2023”, zilitolewa na Chama cha Maofisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST).

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Mawasiliano wa TANAPA, Catherine Mbena, amesema ushindi huo umetokana na mchango mkubwa unaotolewa na idara yake katika kuhabarisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya uhifadhi na utalii.

Amesema idara hiyo imekuwa daraja la kuiunganisha taasisi hiyo na umma, na kwamba tuzo hiyo itakuwa chachu ya kuimarisha uhusiano kati ya TANAPA, serikali, vyombo vya habari na wadau mbalimbali.

“TANAPA sasa ni jicho la nchi kwa kuwa, taasisi inatoa mchango mkubwa wa kuingiza fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi kupitia sekta ya utalii.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa serikali kwa kuongeza hamasa katika sekta ya utalii na kuitangaza kimataifa kupitia Filamu ya The Royal Tour,” amesema.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameipongeza (PRST) kwa kuandaa tuzo hizo ambazo zinachochea uwajibikaji.

Amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari na maofisa uhusiano kwa umma kuongeza ubunifu, weledi na uwajibikaji ili jamiii inufaike kwa kupata taarifa sahihi zinazohusu maendeleo ya taifa.

Amesema tuzo hizo zitasaidia kukuza vipaji na kuongeza chachu kwa wanataaluma akiwataka waandaji wake kutenda haki na kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa.