Wananchi Longido wapongeza maendeleo yanayoletwa na Mgodi wa Mundarara

By Frank Monyo , Nipashe Jumapili
Published at 10:16 AM Mar 24 2024
news
Picha: Frank Monyo
Mnufaika wa mgodi huo Leita Mollel

WANANCHI wanaozunguka mgodi wa Mundarara unaochimba madini ya Rubi uliopo katika kijiji cha Mundarara, Tarafa ya Engarenaibor , Wilaya ya Longido mkoani Arusha wameupongeza mgodi huo kwa kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuwashirikisha katika shughuli za uchimbaji madini.

Hayo yamebainishwa  na wananchi hao kwa waandishi wa habari wanaofanya ziara ya kutembelea mgodi huo kwa lengo la kujionea shughuli za uchimbaji madini.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mgodi huo Leita Molleli amesema kuwa mgodi wa mundarara umekuwa mkombozi katika maisha yao ambapo kupitia mgodi huo wananufaika na huduma mbalimbali.

Akitolea mfano baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kupata ajira, kupata mchanga wa madini,ujenzi wa madarasa , uboreshaji wa makazi kupitia biashara ya madini wanayofanya mgodini hapo.

Kwa upande wake meneja wa mgodi huo Frank Luholela amesema kuwa mgodi unaendelea kutekeleza kanuni ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) hususani katika masuala yanayohusu maendeleo ya jamii.

Luholela ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu  ya uchimbaji, mgodi umeendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi wanaouzunguka kwa kuwapatia mifuko ya mawe ya madini yanayochimbwa katika  mgodi ambapo uchambua na kupata madini ambayo wanauza na kupata kipato.

Akielezea kuhusu maendeleo ya mgodi huo , Luholela ameeleza kuwa mgodi umefikia mita 320 kwenda chini ambapo kwa upande wa magharibi umeenda mita 500 na mashariki mita 100.
 Kuhusu changamoto ya mgodi, Luholela ameeleza kuwa kwasasa changamoto kubwa na mipaka ya chini sababu kunatokea mitobozano katika uchimbaji jambo linalopelekea kushindwa kuendelea na uchimbaji.
Mgodi wa Mundarara ulianza uchimbaji mwaka 2021.