Benki ya NMB yazindua akaunti ya kikundi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:10 AM May 04 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

Benki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi, inayokuja na maboresho makubwa kwa wanakikundi wote kufurahia huduma kidijitali.

Kupitia akaunti hiyo, wanakikundi wataweza kutumia NMB Mkononi, kufungua akaunti kiurahisi na papo hapo kwa kubofya 15066#,kuchangia michango na kukopeshana mikopo ya kikundi kupitia simu zao,kuhamisha fedha kwa wanakikundi bila makato yoyote na kupata taarifa za kikundi kwa uwazi, kwa wakati, na kwa usalama wakati wowote. 

Taarifa hizo ni kama salio, hela ikitolewa, mwana kikundi akikopeshwa, mtu akiongezwa kwenye kikundi na taarifa nyingine,kujiunga na Bima ya Maisha ya Vikundi ya NMB kwa ajili yao wenyewe na wategemezi wao, kidijitali na kuchangia kupitia chaneli zetu zote, kupitia mitandao ya simu au kwa kutumia namba maalum ya malipo, yaani (Control Number).


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jana, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima alisema: “Pongezi ziifikie Menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya NMB kwa kuja na NMB Kikundi Akaunti, ambayo ni suluhisho kubwa na mbadala katika utoaji Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Vikundi vya Kijamii vya Kuweka Akiba na Kukopa. Huu ni zaidi ya ubunifu katika ustawi na maendeleo ya vikundi na wanachama wake.” alisema na kuongeza kuwa: 

“NMB Kikundi Akaunti ni jitihada za wazi za Benki ya NMB katika kusapoti juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imejikita katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha ili kuhakikisha idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki inaongezeka maradufu.”

“Kwa hiyo kuboreshwa na hatimaye kuzinduliwa kwa NMB Kikundi Akaunti – ambayo ni ya pamoja kwa wanachama wa vikundi, ni utekelezaji wa Malengo na Mkakati wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza Ujumuishwaji Wanawake na Makundi Mengine kwenye Hduma Jumuishi za Kifedha na kubwa zaidi usalama wa fedha zao,”


Alisema imeelezwa kuwa NMB Kikundi Akaunti iliyozinduliwa jana sio tu suluhishi ya changamoto mbalimbali za vikundi vya kijamii, bali pia imebeba huduma ya Bima ya Maisha kwa wanakikundi ambao sio lazima wawe na akaunti binafsi ya NMB. "Hili jambo jema na la kibunifu linaloakisi dhamira njema ya benki kwa jamii.” alisema 


Afisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna, alisema maboresho makubwa yamefanyika yaliyotoakana na mrejesho wa wanachama wa vikundi 200,000 vyenye wanachama zaidi ya milioni 1 wa iliyokuwa NMB Pamoja Akaunti tuliyoizindua mwaka 2020 hadi kuwa NMB Kikundi Akaunti iliyozinduliwa jana, akaunti ya kidigitali yenye unafuu, urahisi na usalama katika matumizi yake.

“Ni kutokana na mabadiliko na maboresho hayo, kila mwanakikundi sasa anaweza Kuteleza Kidijitali na NMB Kikundi Akaunti, ikiwemo Kufungua akaunti papo hapo, Kuchangia michango na kukopeshana mikopo ya kikundi, Kuhamisha fedha kwa wanakikundi bila makato na Kupata taarifa za kikundi kwa uwazi, na usalama wakati wote, mahali popote.” alisema na kuongeza kuwa:

“Aidha, NMB Kikundi Akaunti itawawezesha wanakikundi Kuchangia michango ya kikundi bila haja ya vikao wala kutembelea tawi la NMB, Kuangalia salio na taarifa fupi ya kifedha ya kikundi, kubwa zaidi akaunti hii inajumuisha Bima ya Maisha, ikiwapa wanakikundi uhakika wa kifedha na amani ya akili kwa mwanachama na familia yake.”