NBC yakabidhi msaada wa vitanda Shule ya Polisi Moshi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:12 PM Apr 25 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Sehemu ya vitanda 28 vilivyotolewa na benki ya NBC kwa wanafunzi wa kike wanaosoma Shule ya Polisi Tanzania (TPS) iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro ikilenga kuboresha mazingira ya maladhi kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.

Benki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule ya Polisi Tanzania (TPS) iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro ikilenga kuboresha mazingira ya maladhi kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.

Hafla fupi ya makabidhiano ya vitanda hivyo ilifanyika jana shuleni hapo ambapo ilishuhudiwa Meneja wa wa benki ya NBC tawi la Moshi, Lazaro Mollel akimkabidhi Mkuu wa Shule hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Ramadhani Mungi msaada huo kwa niaba ya benki hiyo.

Mollel alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za benki ya NBC katika kuhamasisha suala zima la ulinzi na usalama kupitia ushirikiano wake na jeshi hilo. Hatua hiyo inalenga kutambua mchango wa jeshi hilo katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa jamii ikiwemo benki hiyo na wateja wake.

“Jeshi la Polisi ni miongoni mwa wadau wakubwa wa benki ya NBC hapa nchini. Uhusiano mkubwa uliopo uliopo baina ya taasisi hizi mbili unatokana na kutegemea baina yetu kutokana na majukumu yetu ambapo kupitia huduma zetu za kibenki jeshi la polisi limekuwa likinufaika kupitia huduma za vipaumbele kwao na sisi pia kama benki tumekuwa tukinufaika na huduma za jeshi hili muhimu hususani kwenye suala zima la kuhakikisha ulinzi na usalama kwa benki na rasilimali zake wakiwepo wafanyakazi, fedha na majengo bila kusahau usalama wateja wetu pia,’’ alibainisha.

Mollel aliongeza kuwa ushirikiano baina ya  taasisi hizo mbili pia unaonekana kwenye usimamizi wa ulinzi na usalama wakati wa mechi za mpira wa miguu kwenye ligi mbalimbali zinazodhaminiwa na benki hiyo zikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League), Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship),  Ligi ya Vijana (NBC Youth League) pamoja na mbio za NBC Marathon zinazofanyika kila mwaka jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye hafla hiyo SACP Mungi pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo  alibainisha kuwa shle hiyo inahitaji misaada mingi ya namna hiyo kufuatia ongezeko la wanafunzi ambao kwasasa wapo takribani 5000.

“Wakati shule imehamishiwa hapa Moshi mwaka 1954 ilikuwa na wanafunzi 600 ila kwasasa wapo takribani 5000. Ongezeko hili linakwenda sambamba na ongezeko la mahitaji muhimu ikiwemo mazingira bora ya kuishi na kupumzika kwa wanafunzi, mazingira bora ya kufundishia yaani madarasa na vifaa bora vya kufundishia. Serikali imekuwa ikijitajidi kufanikisha haya yote ila bado tunahitaji jamii pia ione umuhimu wa kuisadia kwenye hil na hiyo ndio sababu tunawashukuru sana NBC kwa msaada huu,’’ alisema.

Akizungumzia msaada huo SACP Mungi alisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba wa vitanda shuleni hapo na hivyo kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo yao wakiwa katika mazingira bora ya kupumzikia.

“Yote haya yanawezekana kufuatia ushirikiano mzuri na wadau wetu mbalimbali ikiwemo benki ya NBC ambayo licha ya kutupatia huduma nzuri za kifedha pia jeshi la polisi limekuwa likiipatia huduma mbalimbali hususani za kiulinzi na usalama kwa rasilimali zake pamoja wateja kwenye matawi yake kote nchini.‘’