Nuru mpya kikokotoo, nyongeza ya mshahara

By Cynthia Mwilolezi ,, Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 03:06 PM May 02 2024
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
PICHA: MAKTABA
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

NI ahadi ya matumaini baada ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango kuzungumzia hoja ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu kuwa imepokewa na kuahidi itafanyiwa uchambuzi zaidi.

Aidha, nyongeza ya mshahara, Dk. Mpango amewataka wafanyakazi kuendelea kutega sikio kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan atasema jambo hivi karibuni.

Ametoa kauli hiyo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa katika Jiji la Arusha, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema serikali imepokea hoja kuhusu kubadilisha kanuni ya kikokotoo kwa wastaafu kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi zaidi kwa kuwa wafanyakazi hawaridhishwi na kanuni hizo.

“Rais Samia Suluhu Hassan, Mama wa Taifa; ameaniagiza niwaambie wafanyakazi wa Tanzania kuwa endapo hali hii itadumu, wafanyakazi wawe na matumaini kwamba atasema jambo hivi karibuni,” amesema.

Kuhusu kodi ya kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi, Dk. Mpango alisema, tayari serikali imeanza utafiti ambao utajumuisha sekta ndogo.

Kutokana na uhitaji huo, Dk. Mpango ametoa wito kwa wajumbe wa bodi kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), kushiriki kikamilifu mchakato huo ili kufikia uamuzi shirikishi utakaosadifu mazingira ya wakati uliopo.

WATUMISHI H/SHAURI

Dk. Mpango amesema kuanzia Julai mwaka huu, watumishi 473 kutoka Halmashauri 101 ambazo zilibainika kutokuwa na uwezo wa kulipa mishahara watumishi wake kwa kutumia mapato ya ndani sasa watalipwa kupitia mfuko mkuu wa hazina.

SSRA KUREJESHWA

Vilevile, Dk. Mpango, amesema serikali imesikia hoja ya kutaka kurejeshwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ikiwa ni miaka mitano tangu ilipovunjwa na majukumu yake kutwaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

“…Ushauri wenu wa kufikiria upya mwaka 2019 tumeupokea na tutaendelea kuutathimini kisha uamuzi utafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu na wa kiuhalisia wa kiuendeshaji kwenye sekta ya hifadhi ya jamii.” amesema Dk. Mpango.

BIMA YA AFYA

Dk. Mpango amesema serikali imefanya maboresho katika orodha ya taifa ya dawa muhimu pamoja na miongozo mbalimbali ya tiba, hivyo kutokana na maboresho hayo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umefanya maboresho katika kitita chake ili kwenda sambamba na miongozo hiyo kwa lengo la kuboresha huduma bora kwa wanachama wake.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, kutokana na changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza utekelezaji wa kitita hicho, serikali iliunda kamati huru ya wataalamu ili kupitia hoja za wadau na kupata suluhu ya changamoto zilizojitokeza.

Amesema kwa kuwa mapitio ya kitita bado yanaendelea, serikali itahakikisha wadau wote muhimu wanashirikishwa kikamilifu katika mchakato huo na kutatua changamoto zilizojitokeza.

KIKOKOTOO

Dk. Mpango alisema: “Serikali imepokea ushauri uliotolewa. Hata hivyo ni muhimu kuzingatia kwamba uendeshaji na usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni suala la sayansi ya watakwimu bima.”

Hata hivyo, alisema serikali inawategemea wataalamu washauri kuhusu suala hilo la uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Amesema serikali iliposhauriwa na wataalamu iliamua kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii Sh. trilioni 2.147 hatua ambayo imeimarisha mifuko hiyo.

KODI YA MSHAHARA

Kuhusu mapato yasiyo ya mshahara, Dk. Mpango alisema: “Naomba nieleze kwamba kodi katika mapato ya wafanyakazi inatozwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa ukokotoaji na ukusanyaji unazingatia kanuni za msingi za utozaji kodi ikiwamo kuweka usawa kwa watu wenye kipato kinachofanana.”

Amesema uratibu huo unawezesha baadhi ya vitendo vya waajiri wasio waaminifu kufanya udanganyifu wa kupunguza kiasi cha msingi cha mshahara na kuainisha kwenye mahesabu yao kiasi kikubwa cha posho na marupurupu ili kukwepa wajibu wa kulipa kodi na masuala ya pensheni za wafanyakazi wao.

NYONGEZA MSHAHARA

Dk. Mapango alisema serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mishahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa waajiriwa. Misingi hii ni muhimu ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la taifa na athari nyingine kwenye utulivu wa deni la taifa kwa ujumla.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, ameitaka serikali kurudisha kitita cha zamani cha matibabu kinacholalamikiwa na Watanzania, ili kumaliza malalamiko kwa wanachama ambao wengi wao ni watumishi wa umma.

Amesema suala la kikokotoo, TUCTA inakiri kushiriki katika mabadiliko kilichokuwa cha asilimia 50 na 25, ambacho walijadili, mara ya kwanza kilienda kwenye asilimia 25 kwa wote.

Amesema jambo hilo kwa wafanyakazi bado lina malalamiko, huku akiiomba serikali kuwaonyesha njia watakayoifuata kwa ajili ya ustawi wa mifuko na malipo hasa ya mkupuo wakati wa kustaafu.

Katibu Mkuu wa TUCTA, Henry Mkunda, alisema pamoja na maboresho ya viwango vya mishahara kufanyika baada ya kusimama kwa miaka sita, bado havikidhi kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Aidha, alisema gharama za maisha zimepanda kunakosababishwa na kupanda kwa bidhaa na vitu vingine muhimu hususani vyakula, matibabu, usafiri, mafuta na vifaa vya ujenzi.