Pinda awageuzia kibao maofisa TRA

By Munir Shemweta , Nipashe
Published at 01:21 PM May 05 2024
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.
PICHA: MAKTABA
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara wa eneo la Majimoto katika Halmashauri ya Mpimbwe, wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Pinda ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha pamoja kati ya maofisa wa TRA Makao Makuu na wafanyabiashara wa eneo la Majimoto, kilichofanyika katika Halmashauri ya Mpimbwe.

Kikao hicho cha siku moja, kilitokana na kuwapo malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na maofisa wa TRA, jambo walilolieleza kuwa limekuwa likisababisha usumbufu katika biashara zao.

‘’Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kavuu, niko tayari kutoa ushirikiano na TRA lakini ushirikiano huo uende sambamba na mamlaka kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara,‘’ amesema.

Pinda amesema ni wajibu wake kuhakikisha maisha ya wafanyabiashara katika eneo hilo yanakuwa rafiki na kusisitiza kuwa eneo hilo linapoteza wateja wengi na sababu ya kuwapo na uhusiano mbovu na walipakodi.

Pia amewataka maofisa wa TRA katika eneo hilo kutokuwa na dharau kwa wafanyabiashara na kuhoji: “Unapomdharau mlipakodi unategemea kitu gani?” Alisisitiza  mamlaka hiyo kutoa huduma nzuri kwa kwa wateja.

Kwa mujibu wa Pinda, lazima maofisa wa TRA wawe rafiki na wafanyabiashara ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kusababisha mkwamo kwa wafanyabiashara.

Amebainisha kuwa TRA pamoja na mambo mengine, lazima ijikite kutoa elimu kwa mlipakodi kama maofisa wake walivyofanya kwa kwenda kwa  wafanyabiashara wa Majimoto huku akiwataka kuacha kabisa siasa katika shughuli za kibiashara. 

‘’Nasema haya ili mje na mageuzi makubwa kwa lengo la kuboresha,” amesisitiza. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe, Shamim Daud, amesema zaidi ya asilimia 50 ya mzunguko wa fedha katika halmashauri yake inatoka eneo la Majimoto ndiyo maana halmashauri imeweka uwekezaji mkubwa katika eneo hilo ili kuhakikisha huduma za jamii zinaimarishwa na kupunguza changamoto kwa watu wanaoingia na kutoka.

‘’Kwa hiyo tunashukuru na tunatumaini kikao hiki watu watakapotoka watakuwa wamejifunza na TRA watakuwa wameelewa changamoto za maeneo hayo na kuwaletea mabadiliko makubwa’’. Amesema Pinda.