Taarifa mikopo ‘kausha damu’ kutua bungeni

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 12:37 PM May 02 2024
Mikopo ‘kausha damu’ kutua bungeni.
PICHA: MAKTABA
Mikopo ‘kausha damu’ kutua bungeni.

SERIKALI inatarajiwa kuwasilisha bungeni taarifa ya kushamiri mikopo ya ‘kausha damu’ kesho, baada ya wabunge kuibua hoja ya kushamiri hadi mitandaoni ikizihusisha baadhi ya kampuni za simu.

Akizungumza bungeni, Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson, amesema serikali inatarajia kuwasilisha taarifa hiyo Alhamisi.

Aprili 24, mwaka huu, wabunge wameibua suala hilo na kuhoji mikakati ya serikali wa kuzibana taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa riba kubwa, hali inayosababisha magonjwa ya afya ya akili na uvunjifu wa ndoa.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni, Mbunge wa Viti Maalum, Felista Njau, amehoji mkakati wa serikali wa kukomesha mikopo ya kausha damu ili kunusuru wananchi ambao wamekuwa wakipata matatizo ya afya ya akili na ndoa nyingi kuvunjika.

Katika swali la msingi, mbunge huyo ametaka kujua kuna mkakati gani ya kufuatilia na kuchukua hatua kwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye riba kubwa kinyume na muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kadhalika, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Shally Raymond, amesema pamoja na Sheria ya BoT ya mwaka 2018 na Kanuni za Mwaka 2019, takribani mikoa 17, ukiwamo  Kilimanjaro hasa wilaya ya Moshi, imekuwa ikitolewa mikopo kausha damu na kutaka kauli ya serikali. 

“Kampuni za simu zimekuwa zikitoa mikopo haraka bila kujaza fomu na vijana na wanawake wajasirimali wa Kilimanjaro wamekuwa wakichangamkia fursa hiyo, Je? lini serikali italazimisha kampuni hizo kutoa elimu?” amehoji.

Kutokana na kauli hizo, Spika Tulia  amesema hana uhakika kama kampuni za simu ambazo zimesajiliwa zinatoa mikopo kausha damu kama taasisi nyingine ambazo hazijasajiliwa.

“Naibu Waziri wa Fedha nakupa muda baada ya kipindi cha maswali katafute habari za uhakika hapo nje kwa kampuni za simu kama zinatoa mikopo kausha damu,”  amesema.

Awali akijibu maswali ya wabunge hayo, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, amezielekeza taasisi zinazotoa mikopo hiyo kuacha mara moja na serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo.

Pia ameagiza BoT kuzifuatilia taasisi zinazoenda kinyume na sheria hiyo, serikali haitakuwa na muhari kwa taasisi zinazokiuka sheria na kanuni hizo.

Kadhalika amesisitiza serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera, kiutawala na kisheria ili kudhibiti tabia ya baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo kinyume na miongozo iliyopo.

Amesema wataendelea kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya fedha ili kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu fursa za mikopo zilizopo, viwango vya riba na athari zake, vigezo vya kuzingatia na umuhimu wa kurejesha mikopo.