Tanzania yanadi mafaniko yake Sekta ya Madini mkutano wa uwekezaji wa madini Malawi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:56 AM Apr 26 2024
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa akizungumzia mafanikio katika Sekta ya Madini.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa akizungumzia mafanikio katika Sekta ya Madini.

Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika Sekta ya Madini kwa kuweka mifumo mizuri na thabiti ya kusimamia Sekta ambayo imepelekea watu wa makundi mbalimbali kufanya uwekezaji kwenye Sekta hiyo.

Dk.  Kiruswa amesema hayo wakati akifanya wasilisho la  Tanzania katika Jukwaa la Kwanza la Madini na Uwekezaji nchini Malawi lililofanyika kwa siku mbili kuanzia Aprili 23 hadi 24, 2024 Mjini Lilongwe, nchini humo.  

Amesema kuwa mafanikio yaliyofikiwa na nchi ya Tanzania kwenye Sekta ya Madini yamepiga hatua kiasi cha kutoa Mchango mkubwa kwenye pato la taifa na kuwa Sekta inayochochea Uchumi wa Taifa na wananchi wake kwa kiasi kikubwa, hatua ambayo imeyavuta mataifa mbalimbali kuhitaji kujifunza toka Tanzania ambapo tayari baadhi ya washiriki wameomba kuja kujifunza nchini. 

Aidha, Dk. Kiruswa ameongeza kuwa, pamoja na Tanzania kuonenekana kupiga hatua kubwa, bado inaendelea na juhudi za kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji ili kufikia malengo makubwa kupitia  Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri.  

Vilevile, amewakaribisha wawekezaji na kampuni zenye nia ya kuwekeza kwenye Utafiti wa Madini na Uongezaji Thamani Madini kuja kuwekeza nchini Tanzania na kutumia fursa hiyo ambayo hivi sasa ni imepewa kipaumbele kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Dk. Steven Kiruswa ameongoza Ujumbe wa Tanzania katika Jukwaa hilo akiambatana na Naibu Katibu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo pamoja na Wataalam kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Tume ya Madini ikiwa ni katika kutekeleza azma ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuonyesha mafanikio ya Sekta ya  Madini ya Tanzania kwa mataifa ya jirani. 

Jukwaa hilo lilizinduliwa Aprili 23, 2024 na Rais wa Malawi Dk. Lazarus Chakwera ambako lilikuwa na kaulimbiu ya “Kubadilisha Taifa kwa Uchimbaji Endelevu wa Madini” ambapo Kiongozi huyo alisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za madini na kuzitaka taasisi za fedha nchini humo kuwekeza katika Sekta ya Madini ili kukuza uchumi wa taifa hilo na kuingiza mapato ya nje. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Dkt. Kiruswa amekutana na Rais Dk. Lazarus Chakwera katika Ikulu ya Malawi  Aprili 24, 2024 kufuatia mwaliko wa Kiongozi huyo Mkuu wa Malawi kwa Mawaziri walioshiriki jukwaa hilo, ambako Dk. Kiruswa amemshukuru Rais Chakwera na kumweleza kuwa Tanzania na Malawi zitaendelea kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Madini kwa manufaa ya pande zote mbili.