TFRA yahimiza matumizi ya mbolea, kilimo cha kisasa

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:54 AM Apr 19 2024
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk. Anthony Diallo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk. Anthony Diallo.

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk. Anthony Diallo amewataka wakulima mkoani Kagera kujikita kwenye kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea, ili kuongeza tija ya uzalishaji kwenye mazao mbalimbali shambani.

Alitoa wito huo wakati wa ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wakulima na mawakala wa usambazaji wa  mbolea za ruzuku wilayani Ngara.

"Nia yetu kubwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi wakulima kwa kuongeza uzalishaji baada ya kutumia mbolea zitakazosaidia kuongeza tija kwenye uzalishaji" alisema Dk. Diallo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent aliwataka wakulima kuwekeza zaidi kwenye kupima afya ya udongo ili waweze kutumia mbolea inayoendana na uhitaji wa udongo.

Alisema matumizi sahihi ya mbolea yanaleta tija kwenye uzalishaji, hivyo aliwasihi wakulima kuendelea kutumia mbolea sahihi kulingana na uhitaji wa udongo wao baada ya kuupima. 

Kaimu Meneja wa chama cha wakulima Ngara, Fadhili Damian Kamhanda alisema Wilaya ya Ngara ilifanikiwa kupokea tani 65 za mbolea sawa na mifuko 1,300 iliyosambazwa kwa wakulima kwa asilimia 98.

Alisema chama chao kiliingia mkataba na kampuni za OCP na Minjingu ili kusambaza mbolea za ruzuku ambapo ni mara ya kwanza kwa mbolea kufikishwa wilayani humo.