NFRA yanunua tani zaidi ya laki 2 za chakula

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:23 PM Apr 25 2024
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde.
PICHA: MAKTABA
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), imenunua na kuhifadhi tani 294,069.216 kwa ajili ya kusambazwa katika maeneo ambayo yatabainika kuwa na upungufu wa chakula, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amesema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kalenga (CCM), Jackson Kiswaga, ambaye alihoji serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la njaa linalosababishwa na upungufu wa mvua.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Silinde amesema nchi imekuwa ikijitosheleza kwa chakula kwa kigezo cha upimaji wa utoshelevu kati ya asilimia 112 na 126 kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.

Pia amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha upungufu wa mvua na kuhatarisha usalama wa chakula, serikali imechukua hatua kadhaa.

Ametaja hatua hizo ni kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kutoka hekta 727,280 msimu wa 2022/23 hadi kufikia hekta 1,200,000 ifikapo 2025.

“Hatua zingine ni kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na usambazaji wa mbolea kwa mpango wa ruzuku na kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya chakula kupitia NFRA kutoka tani 360,000 hadi tani 500,000 ifikapo 2025,” amesema .

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Grace Tendega, amehoji serikali ina mkakati gani wa kudhibiti utaratibu wa wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi kununua mazao nchini kwa fedha taslimu.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema serikali ilitoa tangazo kwa umma Mei 23, 2023 na kuweka utaratibu wa kufuata ili kudhibiti ununuzi holela wa mazao ya kilimo kutoka kwa wanunuzi wanaotoka nje ya nchi.

Silinde amesema utaratibu huo umefafanua hatua za kufuata kwa manunuzi wa mazao kutoka nje ya nchi ikiwamo kununua mazao kupitia mifumo rasmi ya kifedha.

Amesema katika kudhibiti ununuzi holela wa mazao ya kilimo, serikali inaendelea na uandaaji wa kanuni kwa mujibu wa sheria ya usalama wa chakula sura 249 na marekebisho yake ya mwaka 2009 kupitia sheria ya nafaka na mazao mchanganyiko.

“Kupitia kanuni hizo, serikali itaandaa mwongozo kuhusu utaratibu wa uuzaji na ununuzi wa mazao ikiwamo kununua kwenye masoko ya upili pamoja na kusajili wanunuzi wa mazao wa ndani na nje ya nchi,” amesema.

Pia amesema lengo ni kuwatambua, kuwasimamia na kufuatilia shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.