Watanzania washiriki mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza

Nipashe
Published at 01:13 PM May 05 2024
Baadhi wa washiriki wa EATV Jogging wakiwa mazoezini.
PICHA: EATV
Baadhi wa washiriki wa EATV Jogging wakiwa mazoezini.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, jana alishiriki mazoezi ya pamoja ya kampeni ya kitaifa inayoratibiwa na Wizara ya Afya ya kuhamasisha Watanzania kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, maradhi ya moyo na kisukari.

Katika ushiriki wake huo, Majaliwa alisema hatua hiyo pia ni kuunga mkono wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa hayo. Kutokana na kasi ya kufanya mazoezi na kuandaliwa eneo maalumu la Coco Beach, Dar es Salaam kwa ajili ya jambo hilo, Waziri mkuu alilitaka Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi wa eneo hilo ili liendelee kuwa salama.

Programu ya ufanyaji mazoezi ilianzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan na yeye mwenyewe kushiriki na kuwahamasisha watanzania kushiriki mazoezi mbalimbali, huku  akisema moja ya mambo ya kujivunia katika kipindi chake cha miaka mitatu ya uogozi ni mafanikio katika sekta ya michezo.

Wakati hayo yakifanyika, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alibainisha kuwa kutokana na ongezeko la magonjwa 10 yasiyo ya kuambukiza wizara ilileta ombi la kuanzisha utaratibu huo kila Jumamosi.

Waziri Ummy alibainisha kuwa mwaka 2022, kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua Watanzania, moja lililojitokeza ni shinikizo la juu la damu likifuatiwa na kisukari, hivyo kuona kuwa njia mojawapo ya kudhibiti na kupunguza tatizo hilo linalokua kwa kasi ni kuanzisha mpango wa mazoezi. 

Wito wa kufanya mazoezi hivi sasa umekuwa kama wingo usio na mwisho kwani viongozi wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kufanya hivyo ili kupunguza uwezekano wa wananchi kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na mtindo wa maisha. Watu wamekuwa hawafanyi mazoezi au kushiriki michezo hatua ambayo inachochea kuongezeka kwa maradhi hayo. 

Mtu anaweza, kwa mfano, akatoka ndani ya nyumba na kuingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja ofisini na wakati anapoamka hafanyi hata mazoezi au kutembea hatua kadhaa kuupa mwili wake nishati. Akifika kazini, anakaa ofisini mpaka muda wa kumaliza kazi na baadaye kuingia kwenye gari moja kwa moja nyumbani. Hata akifika nyumbani, anakaa na kuangalia televisheni kisha kula na kwenda kulala.

Hata katika shule, hivi sasa hakuna mchakamchaka katika shule nyingi na hata mazoezi yanaonekana ni adhabu kwa wanafunzi. Hata hivyo, serikali inastahili pongezi kwa hivi karibuni kutamka kuwa mchakamchaka ni lazima katika shule zote, ziwe za binafsi au za umma ili kuwaweka katika hali njema kiafya na kuwaepusha dhidi ya maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Kwa hakika, magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni janga linalolinyemelea taifa kutokana na takwimu zinazotolewa mara kwa mara juu ya kuendelea kuongezeka. Kutokana na ukweli huo, suala la mazoezi kwa wananchi wote linapaswa kupewa uzito unaostahili. 

Tunasema hivyo kwa sababu taarifa katika taasisi za afya kama vile hospitali zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kisukari yanazidi kuongezeka huku sababu kubwa zikitajwa kuwa ni mtindo wa maisha wa watu kutokufanya shughuli za kuwafanya watoke jasho kama vile mazoezi na ulaji wa vyakula na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Ni vyema sasa Watanzania wakazingatia maonyo na mashauri ya viongozi na wataalamu wa afya kwa kuzingatia masharti katika ulaji na unywaji wa vileo. Kwa kufanya hivyo, ni dhahiri kwamba maradhi mengi, hasa yasiyo ya kuambukiza yatapungua na hatimaye fedha nyingi zinazoelekezwa kwenye matibabu, kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo.