Agizo la Waziri Ummy litekelezwe kwa vitendo

Nipashe
Published at 11:06 AM Jan 23 2024
 PICHA:
Nipashe
PICHA:

HIVI karibuni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa tamko kwa hospitali zote za serikali zinazozuia miili ya marehemu kuchukuliwa na ndugu zao kwa sababu ya kukosa pesa za kuikomboa.


Agizo hilo la Waziri Ummy linatokana na usumbufu wanaokumbana nao ndugu wa marehemu wanapotaka kuchukua miili ya ndugu zao kwa ajili ya kwenda kuipumzisha kwenye makao yao ya milele.

Tatizo hilo huwakumba ndugu wengi kutokana na kutomudu gharama za kulipia za kuichukua miili hiyo kwa kuwa wanatoka kwenye uuguzaji ambako hutakiwa kulipia huduma na hatimaye ndugu yao anapofariki wanakuwa hawana pesa hizo.

Wananchi wengi wanaishi katika hali ya kipato cha chini na inapotokea ndugu kupata maradhi, humuuguza kwa kuchangishana tena michango yenyewe hupatikana kwa taabu.

Agizo la Waziri Ummy limekuja baada ya ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, kumtaka atolee ufafanuzi wa baadhi ya wananchi kuzuiwa maiti hospitali kutokana na kudaiwa. 

Tatizo hilo limekuwa likiwakera Watanzania wengi kwa hospitali kuzuia miili baada ya ndugu kushindwa kulipa gharama alizokuwa akitibiwa mpendwa wao. 

Katika ufafanuzi wake Waziri Ummy ameeleza kuwa hospitali zote za serikali ni marufuku kuzuia maiti ya Mtanzania yeyote.

Maelekezo hayo ni ya serikali na yeye akiwa waziri mwenye dhamana amesisitiza hasa kwa kuzingatia misingi ya dini ambayo mtu akifariki anatakiwa kuzikwa siku hiyo hiyo.

Waganga wafadhili wa hospitali zote za serikali wametakiwa kuzingatia miongozo ya kutozuia maiti watafute njia nyingine ya kuruhusu ili ndugu waende kuzika watakapomaliza wataenda kudaiana mambo mengine. 

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Makonda ambaye alifarijika na majibu hayo aliweza umuhimu wa wananchi kupatiwa huduma muhimu kwa kuwa bila wao hakuna kiongozi anayeweza kuwa madarakani kwa sababu wanachaguliwa kupitia vyama na wapiga kura ni wao. 

Wananchi hao wakati mwingine hulazimika kuuza mali zao ili kuwatibu ndugu zao na agizo hilo likitekelezwa litaleta faraja kwa wananchi. 

"Kwa kuwa mimi ni msemaji nitahakikisha hakuna mwananchi atakayeteseka ukishafiwa kwanza ni pigo wengine wanafiwa na baba zao, mama ama mtoto hawezi kuwapata tena tunaishukuru serikali," 

Waziri Ummy alionya kuwa baadhi ya watumishi wa afya kutozingatia maelekezo ya maadili na miongozo mbalimbali katika kutoa huduma za afya.

Kauli yake ni kwa watumishi wa afya wanaokwenda kinyume na miongozo na maelekezo ya serikali kuchukuliwa hatua mara moja na viongozi wa mikoa na wilaya pale watakapobainika kufanya uzembe. 

Alikiri afya ni jambo kubwa na ni gumu, linabadilika na wanaendelea kuongeza msuli kusimamia sekta ya afya kwa kuitaka mikoa na wilaya kuwajibika kwa mambo yote yanayotokea katika mikoa yao na wilaya zao. 

Watumishi wa afya wa hospitali ambao hawana lugha nzuri wanapotoa huduma kwa wajawazito na wengine wakiwa bize kwenye simu badala ya kuhudumia wananchi wanatakiwa kuchukuliwa hatua mara moja. 

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Japhet Simeo, alisema tayari jambo hilo limelifanyiwa kazi.

Kwa hili agizo la Waziri Ummy, tuna imani sasa hakutakuwa na malalamiko ya wananchi kuzuiliwa miili ya ndugu zao.