Makonda aanza na maagizo sita

By Allan Isack , Nipashe
Published at 11:02 AM Apr 09 2024
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda (katikati), akizungumza na umati wa wakazi wa Jiji la Arusha, waliofika kumpokea nje ya ofisi za mkuu wa mkoa huo.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, John Mongela na kuahidi kuanza na mambo sita atakayoanza nayo kazi.

Vile vile, ametoa miezi mitatu kwa Idara ya Ardhi, Ofisa wa Mipango miji kuondolewa na kuagiza watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufuatilia madai ya rushwa badala ya kuwasubiri viongozi wa siasa kuwaagiza kuchunguza. 

Amesema ana mambo sita ya harakaharaka ambayo anaamini yapo katika ilani na serikali ni kuweka msingi wa haki.

“Nitakuwa kiongozi wa kutenda haki sitajitendea haki mimi mwenyewe na uzao wangu bali wananchi wanaodhulumiwa, kunyanyaswa, kucheleweshewa haki zao mimi nimekuja kusimama kwa niaba yao. Kama kuna mtu yupo Ngaramtoni ama kokote, ili mradi una haki yako na unajua ni haki yako sitaangalia kama hujasoma ama hauna hela, ndugu mwenye mamlaka nitasimama katika nafasi yangu kutetea haki yenu.”  

“Mmenifurahia sana ila tutageukana muda si mrefu, sitajali wewe ni nani, baba yako ni nani, ulipataje hicho cheo ama ulihonga kupata hiyo nafasi, asa kama mnasema huyu alikuwa Mwenezi ametoka atakuja amepoa kuna watu wanasema sasa hivi atakuwa amejifunza, hakuna nilichojifunza zaidi ya kuwashughulikia wazembe, wavivu na wala rushwa sina elimu yoyote mimi, hata niwe mksuu wa mkoa wa siku moja inatosha, lakini awepo mtu mmoja ambaye anajua kuna mwanaume alipita hapa,” amesema.

Aidha, amesema jambo la tatu ni ulinzi na usalama na ataendelea kukazia kuhakikisha Arusha inakuwa salama wanapatikana watalii wengi haitakuwa vizuri wasikie mkoa haupo salama. Pia, mji unatakiwa kuwa msafi na wenye nyumba wanatakiwa kupaka rangi ili upendeze.

UTALII

“Jambo la nne ni la utalii na Rais Samia Suluhu Hassan, amesema tutalivalia njuga kweli kweli. Utalii wetu upo katika maeneo matatu tuwe na utalii wa mikutano, nilikuwa nacheki idadi ya watalii hapa mkoani wana idadi yao na TTB na wenyewe wana idadi yao, hizi idadi hazioani maana yake kuna shida mahala.”  

Ameahidi kupita katika wilaya zote sita na kuwasikiliza wananchi kero zao na baada ya kuzichukua watakaa na chama na kuweka vipaumbele vya msingi kwa ajili ya kujibu haja za wannachi kwa mujibu wa maelekezo ya ilani.

Amesema anahitaji ushirikiano wao wanataka kutumikiwa kwa namna gani, bahati aliyokuwa nayo anaweza kuwa kiongozi wa aina yoyote ni kitu pekee ambacho anamshukuru Mungu.

Amesema wakitaka Arusha ibadilike uwe mji wenye amani na utulivu, mwananchi anaweza kusahau mahala simu yake na kuikuta, uwe mji wa kibiashara watu hawafungi maduka saa 11 jioni wanakesha kama ilivyo Kariakoo na barabara zipitike kwa lami, inawezekana.

"Chochote mtakachokitaka kitakuwa kwa sababu kubwa mbili kwa kumtanguliza Mungu na jambo la pili ni kwa kuwa Rais Samia anaipenda Arusha mpaka akamtoa mwanawe kwenye Uenezi na kumleta Arusha kuwa mkuu wa mkoa, huo ni upendo wa namna gani jamani," amewahoji wananchi.

Aidha, amesema wanataka kujenga demokrasia ya kweli, uhuru wa kuandamana na siku nyingine wamualike katika hayo maandamano na atashirikiana nao vizuri. 

Kiongozi huyo alisema kuwa bila maombi asingekuwapo, kwa kuwa katika ziara zake za uenezi amekoswa mara tatu kupoteza maisha na kwamba anawashukuru viongozi wote wa dini wanaoendelea kumwombea. 

“Eneo linalonuka rushwa katika nchi hii ni kwenye ardhi, kama hapa Arusha tunaacha mipango miji tumezalisha ujenzi holela, kuna rushwa pale...hatuna ‘plan’ halafu kuna mtu anaitwa ofisa mipango miji…”

"Haiwezekani akaendelea kukaa hapa mji wa kitalii tunajenga holela, hatumhitaji mtu wa aina hiyo akija ofisini utasikia hivi viwanja ni ‘potential’ msije kuhangaika kunitafutia kiwanja, hangaika kuwahudumia wananchi.” 

Amesema hata watalii wanapofika wanashangaa mji wa kitalii hakuna mipango miji na kuwatumia salamu watu wa ardhi kuwa kama hawasimamii upangaji mji, atawapangia.

Ameagiza pia ndani ya miezi mitatu apatiwe ripoti ya migogoro ya ardhi iliyotatuliwa na mazingira yaliyowekwa kutojitokeza tena kwa migogoro hiyo. 

Aidha, amesema hataki kusikia anaielekeza TAKUKURU kuchunguza rushwa kwa kuwa ni wajibu wao na endapo hilo likijitokeza, atawasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Hamduni, amuondoe mtumishi wake.

Amesema yeye ni Mwenezi aliyevunja rekodi kukaa katika kipindi kifupi (siku 162) kwenye historia, lakini hakuna Mwenezi aliyekaa miezi mitano na kutembea kilometa 11,593, mikoa 23 na kufanya mambo makubwa ambayo hayawezi kufutika kama alivyofanya yeye. 

“Sio muda gani uliokaa, bali umeacha alama gani, kwa hiyo hata hapa sitaangalia muda, hapa naona kama nimechelewa kuanza kazi huu muda nilitakiwa niwe ‘site’ nina kiu ya kuwatumikia wananchi,” amesisitiza. 

Awali, katika mapokezi yake Makonda aliwasili Uwanja wa Ndege Arusha (Kisongo), majira ya saa 4:30 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Precision Air 5H-PWE.

Msafara wake kuelekea ofisi za makao makuu ya mkoa huo, uliongozwa na magari zaidi ya 100 baadhi yakiwa ya kifahari.

Waendesha bodaboda na bajaji walipamba msafara huo huku mamia ya wananchi wakiwa wamesimama pembezoni mwa barabara kutoa uwanja wa ndege kueleka Arusha mjini wakimpungia kwa ishara ya kumkaribisha kwenye mkoa huo.

Kiongozi huyo hakupanda gari la serikali bali alitumia moja ya gari yanayotumika kubeba watalii kwenye msafara huo lenye namba za usajili T625 EDP, akiwapungia mkono wananchi akiwa na familia yake mke na mtoto wake.

Akiwa katikati ya Jiji la Arusha, alipita barabara ya Soko Kuu la Arusha na wafanyabiashara walisimamisha shughuli zao kwa muda kumlaki huku msafara wake ukisababisha msongamano wa magari ndani ya jiji hilo baada ya vyombo vingine vya usafiri kusimamishwa kwa muda.

Akiwa jijini humo, alipita barabara ya stendi kuu ya mabasi Arusha na baadaye kuelekea katika ofisi za Mkoa wa Arusha kwa ajili ya utaratibu wa makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkao wa Arusha, John Mongela, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara.

Makonda alifika ofisini saa 5:30 asubuhi akisubiriwa kwa shauku na wananchi eneo la kiwanja ofisi pamoja na viongozi wa chama na serikali kutoka ngazi mbalimbali.

MONGELA

Mongela amesema Makonda ni ndugu yake na mafanikio atakayoyaleta Arusha yatamgusa moja kwa moja na yupo tayari kumpatia ushirikiano kwa kila jambo.

"Makonda ni mstaarabu, muungwana, lakini ukweli ni kwamba akisema leo anataka litokee, ndugu zangu msije kusema mbona Mongela alikuwa anatubembeleza, hapana nafikiri sasa ni muda wa mkoa kukimbia tumpe ushirikiano wa kutosha haya ni maendeleo yetu sote," amesema Mongela. 

Alikumbusha kuwa mwaka huu kuna uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwataka wananchi wakiunge mkono Chama Cha Mapinduzi ili kukamilisha maendeleo zaidi anachokiahidi wataendesha siasa za kistaarabu za kiungwana na kukifanya chama kupata ushindi.