RC awaonya vijana mijadala isiyo tija

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 07:38 AM Apr 27 2024
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka.

MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amewataka vijana kujiepusha na mijadala yenye nia ovu ya kuwagawanya Watanzania na kuhatarisha Muungano.

Mtaka aliyasema hayo wakati wa mkesha wa maadhimisho ya  miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliofanyika viwanja wa stendi ya zamani mjini hapa. 

“Ni vizuri wakati wote vinywa vya vijana wote wa leo vizungumzie maendeleo, vizungumzie uchumi, vizungumzie kujenga taifa ambalo litathubutu kuwa taifa shindani katika Tanzania ya kesho huko duniani,” alisema.

“Tufanye hivyo kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kwenye hotuba kuwakumbusha wanasiasa na Watanzania vinywa vyetu vijenge Muungano wetu, mahubiri yetu tuhubiri maendeleo yetu kama taifa,” alisema na kuongeza kuwa vijana wanapaswa kuona mipaka iliyopo nchini kuwa ni fursa.

Mkoa wa Njombe pia umefanya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano kwa kupanda miti katika chanzo cha maji Nyikamtwe kilichoko mjini Njombe.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mtaka aliwataka wananchi mkoani Njombe kujiepusha na uchomaji moto, vitendo  ambavyo vimetajwa kusababisha hasara na kukatisha tamaa.

“Tumeshuhudia hasara nyingi sana kwenye wilaya ya Njombe kwa sababu ya uchomaji ambao zaidi unasababishwa na visasi, makusudi au bahati mbaya mtu anaenda kusafisha shamba lake mabua anachoma moto unamshinda. Matokeo  yake unaunguza maekari ya watu ambao wamewekeza kwa muda mrefu,” alisema Mtaka.

Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari, alisema mkoa huo ni wa pili kwa upandaji miti na utunzaji wa mazingira.

Ofisa Misitu Wilaya ya Njombe, Audatus Kashamakula, alisema  miti 1,000 imepandwa katika chanzo cha maji Nyikamtwe.

Nao baadhi ya wanafunzi ambao wameshiriki upandaji miti, walisema wameshiriki maadhimisho ya Muungano kwa kupanda miti rafiki kwa vyanzo vya maji sambamba na kujifunza umuhimu wa kutunza mazingira.