UNFPA yazindua awamu ya pili mradi wa kulinda vijana uitwao SYP

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:37 PM Apr 18 2024
Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Mark Bryan Schreiner, akizungumza katika mkutano huo.
Picha: Sabato Kasika
Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Mark Bryan Schreiner, akizungumza katika mkutano huo.

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, amekemea mtindo wa baadhi ya vijana wanaopata ajira na kuwa na dharau na kujiona wako juu kuliko wengine.

Katambi amesema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa kulinda  vijana nchini. Mradi huo uitwao Safeguard Young People Programe (SYP),   unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Tanzania kwa ushirikiano  na Ubalozi wa Uswis nchini na serikali ya Tanzania.

"Mradi huu ni muhimu kwa vijana wetu, kwani unalenga kuwalinda na pia kuwaandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi," amesema Katambi.

Ameongeza kusema; "Baadhi ya vijana wamekuwa wakiajiriwa na kutaka wanyeyekewe na kujiona wako juu badala ya kutumikia wananchi, mtindo huo wa kunyanyua mabega juu na kuringia watu badala ya kuwahudumia sio mzuri."

Katambi amesema, ni muhimu kila kijana anayepata ajira afanye kazi yake kwa weledi kwa kuwa ajira ni kama dhamana tu, na kwamba kila kijana atumikie taifa lake vizuri.

Naibu waziri Patrobas Katambi (kushoto), Balozi wa Uswis nchi Didier Chassot (katikati) na Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Mark Bryan Schreiner wakiteta PICHA: SABATO KASIKA

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Tanzania, Mark Bryan Schreiner, amesema mradi huo unatekelezwa katika nchi zaidi ya 10 barani Afrika, ikiwamo Tanzania, Rwanda, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Eswatin, Lesotho na Afrika Kusini.

Amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na serikali kusaidia vijana kujitambua na kulinda afya kwa kuepuka vitendo ambavyo ni hatarishi kwao, na kwamba kinaendelea kuunga mkono juhudi za serikali kusaidia kundi hilo.

"Awamu ya kwanza ya mradi huu ilianza mwaka 2022, umekuwa na mafanikio makubwa, na sasa tunazindua awamu ya pili ambayo itakwenda hadi mwaka 2026," amesema Schreiner.

Balozi wa Uswisnchini, Didier Chassot amesema, Uswisi, kama mshirika wa serikali ya Tanzania, inatambua changamoto zilizopo kutokana na kasi ya ongezeko la watu nchini  hasa kwa vijana.

Baadhi ya vijana wakiwa katika mkutano. PICHA: SABATO KASIKA

 "Changamoto hizi ni za kiafya, hasa kuhusiana na masuala ya uzazi na lishe kiuchumi, hasa kutokana na ukosefu wa ujuzi wa kutosha na unaohitajika katika ajira; na hata za kisaikolojia na kijami," amesema Chassot.

Amesema, changamoto hizo zina uzito mkubwa, kiasi kwamba zinaweza kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa miaka ijayo, na kwamba zinatakiwa kutatuliwa haraka.

"Nimeambiwa kuwa kamati ya uongozi ya kanda ya SYP, Botswana mwezi uliopita, Tanzania iliunukiwa tuzo ya nchi iliyofanya vizuri zaidi kati ya nchi 12 zenye mradi wa SYP katika kipengele cha jnsia na uzazi katika afua za uwezeshaji wa kiuchumi na kushughulikia  changamoto zinazowakabili vijana," amesema.

Ameongeza kusema; " Nitakuwa mchoyo wa fadhila, endapo sitachukua fursa hii pia, kuzipongeza Serikali za  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kupitia programu ya SYP, tumeona ni jinsi gani zina nia ya kuwakwamua vijana kimaendeleo."