Wananchi wa Idunda waomba kujengewa daraja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:48 PM Apr 29 2024
Waazi wa Idunda waomba kujengewa daraja.
PICHA: MTANDAO
Waazi wa Idunda waomba kujengewa daraja.

WANANCHI wa Kijiji cha Idunda, Kata ya Kimala, mkoani Iringa wamemuomba Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga kusaidia ujenzi wa daraja ambalo limekuwa likihatarisha maisha yao hasa kwa watoto.

Wamesema hayo katika ziara ya Mbunge huyo, aliyofanya kwaajili ya kuangalia maeneo yasiyopitika ili yarekebishwe.

Wamesema sio tu kwa sababu ya mvua, bali tatizo hilo ni la miaka mingi, eneo hilo halina daraja imara, jambo ambalo limekuwa likikifanya kijiji chao kuwa kama kisiwa.

"Kila siku wanafunzi wa Sekondari wanavuka hapa kwenda na kurudi kutoka shule, daraja halipitiki, wajawazito wanapita hapahapa na matumbo yao, ukivuka maji yanafika juu ya kiuno, tunaomba msaada," amesema mkazi mmoja wa eneo hilo.

Juma Salum (87) mkazi wa Idunda amesema licha na umri wake mkubwa, naye hulazimika kuvuka kwenye eneo hilo, jambo ambalo ni hatari.

"Nikitoka kwenda kutibiwa lazima nivuke kwenye haya maji, wakati mwingine yanakushinda nguvu lakini utafanyaje? Niombe watutengenezee daraja," amesema Salum.

Kutokana na hali hiyo, Nyamoga amewataka Wakala wa Barabara Vijini (Tarura) kutenga fedha za dharura kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

"Tusingoje mpaka mtu azame, apoteze maisha ndio tuje kutengeneza daraja hili, tutengeneze mapema kwa sababu kilio hiki ni cha muda mrefu," amesema Mbunge huyo.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Tarura Wilaya ya Kilolo, Edward Chacha amesema changamoto hiyo wataifanyia kazi ili daraja liweze kujengwa.