Absa yaahidi kuendeleza Dar City Marathon, zafana

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 09:14 AM May 06 2024
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga (kushoto), akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za nusu marathon (Km. 21) za Absa Dar City Marathon kwa upande wa wanaume, Dickson Paul kutoka Mwanza.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga (kushoto), akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za nusu marathon (Km. 21) za Absa Dar City Marathon kwa upande wa wanaume, Dickson Paul kutoka Mwanza.

WAKATI Absa Dar City Marathon 2024, zikitimua vumbi lake jijini Dar es Salaam jana, katika hali ya hewa ya utulivu baada ya tishio la kimbunga Hidaya kupoteza uwezo wake kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka husika, wadhamini wakuu wa mbio hizo Benki ya Absa Tanzania, wameahidi kuendeleza udhamini wao.

Ikiwa ni mara ya nne kufanyika mbio hizo chini ya udhamini mkuu wa Benki ya Absa Tanzania, mtifuano huo ulishuhudiwa wanariadha zaidi ya 3,000 wakifukuza upepo katika mitaa ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam huku lengo lake likiwa ni kusaidia upatikanaji wa vifaatiba kwa ajili ya wodi ya wanawake ya Hospitali ya Mnazi Mmoja pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vipatikanavyo katikati ya jiji hilo.

Akizungumza baada ya kufanyika mbio hizo, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga, alisema kutokana na mafanikio ya mbio hizo, benki hiyo itaendelea kuwapo kwa kipindi kirefu katika kudhamini mbio hizo.

“Kama ahadi ya chapa yetu isemayo 'Tunadhamini Story Yako', Benki ya Absa itaendelea kuthamini stori za maisha ya Watanzania, kwani sehemu ya mapato ya mbio hizi yatakwenda kusaidia jamii kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaatiba kwa ajili ya wanawake na watoto.

“Absa tunaamini kuwa mtu yeyote anaweza kuandika stori yake kutokana na mazoezi na kukimbia ni moja ya mazoezi, lakini pia tunaamini utajiri upo kwenye afya, na kukimbia kunaleta afya. Jamii na nchini itapiga hatua kubwa ya kimaendeleo kukiwa na watu wenye afya bora, Absa tupo kuhakikisha stori hizo zinaandikwa kwa ufanisi,” alisema Luhanga.

Akizungumza kuhusu huduma zao za kibenki, Luhanga alisema benki yao imesheheni bidhaa na huduma mbalimbali zenye ubora wa kimataifa ikiwa ni pamoja na akaunti za watoto, mikopo ya nyumba, magari pamoja huduma ya kadi ya mkopo (credit card), ya kipekee nchini inayomwezesha mteja kupata kadi hiyo ikiwa tayari imewekewa kiasi cha pesa cha kuanzia.

Naye Mwenyekiti wa The Runners Club, waandaaji wa Absa Dar City Marathon, Godfrey Mindu, aliishukuru Benki ya Absa pamoja  na wadhamini wengine kwani kujitoa kwao kunaenda kuleta mabadiliko makubwa kwa maisha ya Watanzania.

Dar City Marathon 2024 ilishirikisha mbio za Km. 5, 10 na 21 huku kwa upande wa Km. 10 wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Anastasia Dolomongo kutoka Arusha akitumia muda wa dakika 34:04:31. Kwa upande wa wanaume mshindi alikuwa Emanuel Shahanga kutoka Hanang akitumia muda wa dakika 29:00:03.

Mbio za Km. 21 (nusu marathon), upande wa wanawake, ushindi wa kwanza ulienda kwa Sara Ramadhani kutoka Arusha pia akitumia muda wa saa 1:13:21:08, huku kwa upande wa wanaume, Dikson Paul kutoka Mwanza akiibuka kidedea kwa kutumia muda wa saa 1:02:58:04.

Mbali na Benki ya Absa kama mdhamini mkuu, wadhamini wengine ni Kampuni ya Alliance Life Assurance, Hill Water, Kilimanjaro Milk na Kampuni ya Garda Security.